Serikali imesema itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kuhakikisha inaboresha afya za mifugo na upatikanaji wa madawa kwa wakati ili wafugaji waweze kunufaika na mifugo yao.
Akizungumza mara baada ya kukutana na Mkurugenzi wa Taasisi ya ZOETIS A.L.P.H.A katika Bara la Afrika Dkt. Gabriel Varga ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema ili kufuga kisasa ni muhimu kwa wafugaji kushirikishwa na wataalamu katika kutambua magonjwa ya mifugo yao na kupatiwa elimu ya namna ya kuwahudumia mifugo.
Ameongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imejipanga vyema katika katika kutekeleza majukumu yake kwa vitendo ili kuhakikisha matokeo chanya yanapatikana katika sekta ya mifugo nchini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah akiwa katika mazungumzo na Dkt. Varga amesema taasisi hiyo ambayo katika bara la Afrika inafanya kazi na taasisi ya Bill and Melinda Gates (BMGF), malengo yao yanafanana na mikakati ya wizara katika kuhudumia ukuzaji viumbe kwenye maji hivyo wizara inatarajia katika kipindi cha miaka miwili au mitatu itafanya kazi na taasisi hiyo ya ZOETIS A.L.P.H.A. katika sekta ya uvuvi.
Dkt. Tamatamah amefafanua kuwa ufugaji samaki kwa sasa hapa nchini unawekewa kipaumbele katika kuendeleza na kuongeza uzalishaji wa samaki kwa kuwa mahitaji ya ulaji wa samaki yameongezeka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya ongezeko la idadi ya watu.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya ZOETIS A.L.P.H.A katika Bara la Afrika Dkt. Gabriel Varga amewaambia makatibu wakuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Elisante Ole Gabriel anayeshughulikia Mifugo na Dkt. Rashid Tamatamah anayeshughulikia Uvuvi, kuwa taasisi yake inatarajia kuanzisha maabara hivi karibuni katika mikoa ya Iringa, Dar es Salaam, Mwanza na Morogoro ili kuboresha afya ya wanyama.
Aidha. Dkt. Varga amefafanua kuwa taasisi hiyo ambayo kwa sasa inahudumia nchi zaidi ya 100 kote ulimwenguni imekuwa ikiwasaidia wafugaji wa bara la Afrika kwa kuwapatia elimu ya huduma ya wanyama ili waweze kufuga kwa tija.
Mazungumzo hayo yamehudhuiriwa pia na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Dkt. Hezron Nonga, Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji Dkt. Nazael Madala na Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania Dkt. Bedan Masuruli wote kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Mwisho.
Imetolewa: Kitengo cha Mawasiliano serikalini
Wizara ya Mifugo na Uvuvi
0 comments:
Post a Comment