Simbaa SC imeendelea kuwapa raha mashabiki wake baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Singida United kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, Miraj Athumani ‘Madenge’ au Sheva dakika ya 39 akimalizia pasi ya kiungo Muzamil Yassin.
Kwa ushindi huo, Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Patrick Aussems inafikisha pointi 18 katika mchezo wa sita ikiendeleza rekodi ya ushindi kwa asilimia 100.
Hali ni mbaya kwa Singida United ambayo leo imepoteza mechi ya tano kati ya nane, nyingine tatu zote ikitoa droo, hivyo kuendelea kushika mkia.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Ruvu Shooting wameibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC bao pekee la Moses Shaaban dakika ya 68 akimalizia pasi ya Abdurahman Mussa dakika ya 27.
Nayo Biashara United ikaichapa 1-0 Namungo FC, bao pekee la Juma Mpakala dakika ya 72 Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara.
Coastal Union wakaibuka na ushindi wa ugenini wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Lipuli FC Uwanja wa Samora, Iringa bao pekee la Andrew Simchimba dakika ya 27.
Mwadui FC ikaongoza kwa 2-0 hadi dakika ya mwisho kwa mabao ya Gerrald Mdamu dakika ya 21 na Hassan Kapalata dakika ya 39, kabla ya JKT kutumia dakika za majeruhi kupata sare ya 2-2 kwa mabao ya Edward Songo dakika ya 90+1 na Najim Magulu dakika ya 90+3.
Kikosi cha Singida United kilikuwa; Mkumbo Msafiri, Gerge Wawa, Gilbert Mbweni, Daudi Mbweni, Meshack Kibona/ Himid Suleiman dk89, David Nartey, Elinyeswia Sumbi, Jonathan Daka, Paschal Ndaga, Stephen Opoku na Ismail Ally/ Emanuel Manyama dk46.
Simba SC; Aishi Manula, Haruha Shamte, Gardiel Michael, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Said Ndemla, Deo Kanda/Rashid Juma dk72, Muzamil Yassin, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu na Miraj Athumani ‘Madenge’/ Gerson Fraga dk78.
Chanzo- Binzubeiry blog
0 comments:
Post a Comment