Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, amewaonea huruma wakazi wa Ubungo kwa kile alichokieleza kuwa hawakuchagua viongozi sahihi, ambao wangeweza kutatua kero zao hii ni baada ya kufika katika eneo maalumu lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya wilaya, bila kuwaona wabunge,pamoja na Meya wa Halmashauri hiyo.
Hayo ameyabainisha Oktoba 29, 2019, alipotembelea eneo ambalo litajengwa hospitali hiyo inayotarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu, ujenzi utakaosimamiwa na Jeshi la kujenga Taifa (JKT), utakaogharimu kiasi cha Shilingi bilioni 1.5.
''Kama nilivyosema juzi, Ubungo hatujapata viongozi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, tumepata kwa ajili ya matumbo yao na ndio maana nimefika hapa nikawa nawatafuta, Meya, Mbunge wa Kibamba na Ubungo yuko wapi, hayupo,sasa niwasihi wakati mwingine msiwaonee haya walafi na wanaonenepa kupitia pesa zenu, wakati wao wameshindwa hata kupaza sauti ili ninyi muweze kupata huduma bora, nafahamu kuna baadhi ya maeneo Ubungo yana changamoto ya barabara, lakini wabunge wenu wala Meya wenu hawana chochote cha kuongea lakini utawakuta wamehamia twitter'' amesema Makonda.
Kufuatia hali hiyo Makonda amewaomba wakazi wa Ubungo, katika kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa, wahakikishe wanachagua viongozi wanaojitambua na watakaoweza kuwasilisha vyema kero zao ngazi za juu.
Oktoba 26, 2019, wakati wa upokeaji wa ndege mpya Dreamline ya pili, Makonda aliwasilisha ombi la kutengewa fedha hizo, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, aliridhia ombi hilo na kuagiza zitengwe shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.
0 comments:
Post a Comment