Saturday, 26 October 2019

Watatu Kizimbani kwa Kukutwa na Tausi wa Ikulu

...
Watu watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu wakikabiliwa na mashtaka matano likiwemo la  kukutwa na ndege watatu aina ya tausi waliokuwa Ikulu wenye thamani ya zaidi ya Sh3.4milioni.

Washtakiwa hao wanaokabiliwa na kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 116/2019 ni David Graha, Mohamed Hatibu na Mohamed Ally.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Vick Mwaikambo, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alisema  Juni Mosi 2015 na Oktoba 14, mwaka huu jijini Dar es Salaam, washtakiwa walijihusisha na mtandao wa uhalifu ambapo wanadaiwa kuratibu genge la uhalifu wakijihusisha na biashara ya ndege aina ya Tausi bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Katika shitaka la pili, Nchimbi amedai katika tarehe hizo washitakiwa walikutwa na ndege watatu aina ya tausi wenye thamani ya USD 1,500 ambazo ni sawa na Sh milioni 3.4 mali ya serikali bila kuwa na kibali.

Pia Oktoba 14, mwaka huu maeneo ya Mikocheni jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Ally alikutwa na ndege watatu aina ya Tausi wanaopatikana Ikulu, ambao aliwapata kwa njia zisizo halali huku katika shtaka la tano, washtakiwa i Graha na Hatibu katika tarehe hizo hizo walijipatia Sh 300,000 huku wakijua fedha hizo ni mazalia ya kosa la wizi.

Hata hivyo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuzingatia kwamba mashitaka hayo hayana dhamana.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 7 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa walirudishwa rumande kwa sababu mashitaka hayo hayana dhamana.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger