WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo Oktoba 26, 2019 anatarajiwa kumwakilisha Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika Mkutano wa 18 wa Wakuu wa nchi na Serikali wa nchi zisizofungamana na upande wowote (NAM) kutoka Afrika na kwingineko duniani utakaofanyika Baku, Azerbaijan.
Mkutano huo unalenga kujadili namna ya kutatua changamoto za kisiasa, kiuchumi na kijamii zinazokabili nchi wanachama wa NAM katika nyakati za sasa, pamoja na na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maslahi ya nchi wanachama wa umoja huo.
Waziri Mkuu aliwasili nchini Azerbaijan jana (Ijumaa, Oktoba 25, 2019) na alipokelewa na Naibu Waziri Mkuu wa Azerbaijan, Bw. Ali Ahmadov pamoja na viongozi wengeine wa Serikali hiyo. Mapokezi hayo yalifanyika katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Heydar Aliyev.
Ajenda za mkutano huo ni kupokea ripoti za mkutano wa maandalizi wa Mawaziri, kupokea ripoti ya mkutano wa maandalizi wa Maafisa Waandamizi, uchaguzi wa nchi zitakazokuwa wajumbe katika ofisi ya uratibu wa shughuli za NAM, New York kwa kipindi cha mwaka 2019-2022.
Mbali na ajenda hizo, pia ajenda nyingine za mkutano huo ni kupokea ripoti za shughuli za umoja huo zilizotekelezwa chini ya Mwenyekiti wa NAM, Venezuela, mjadala mkuu, pamoja na kupitisha maandiko yatokanayo na mkutano.
Mheshimiwa Majaliwa ameambatana na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika ya Mashariki, Dkt. Damasi Ndumbaro na Balozi wa Tanzania Nchini Urusi ambale pia ni Balozi wa Azerbaijan, Meja Jenerali Mstaafu, Simon Mumwi.
Awali, Waziri Mkuu alikuwa Sochi nchini Urusi ambako pia alimwakilisha Rais Dkt. John Magufuli katika Mkutano wa Uchumi kati ya Urusi na Afrika (Russia - Africa Economic Forum) na baadae Mkutano wa wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Mataifa ya Afrika uliofunguliwa na Rais wa Urusi Vladimir Putin.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, OKTOBA 26, 2019
0 comments:
Post a Comment