Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, inaendelea kusikiliza kesi 3,372 zilizosajiliwa Mahakamani hapo kwa sasa, zikiwamo za madai, jinai na ardhi.
Hayo yamesemwa na Naibu Msajili Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Joachim Tiganga, wakati akitoa elimu kwa umma kuhusu utoaji wa huduma zinazotolewa na mahakama hiyo, uliofanyika leo, Oktoba 2, mwaka huu katika ukumbi wa Mahakama Kuu, uliopo jijini Dar es Salaam.
Mhe. Tiganga alisema lengo la kutoa elimu hiyo kwa wananchi ni kueleza huduma zinazotolewa na mahakama hiyo pia kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa wateja wao.
Akifafanua kuhusu kesi hizo, alisema kesi zinazoripotiwa kwa wingi ni kesi za madai ya kawaida ambazo ni 2,169 zikifuatiwa na kesi za jinai 789, wakati kesi za ardhi ni 354.
“Hivyo kutokana na idadi hiyo ya kesi, jaji mmoja anasikiliza kesi zipatazo 450 kwa mwaka badala ya kesi 220 kutokana na kuwepo kwa idadi ndogo ya majaji” alisema.
Aliongeza kuwa Mahakama hiyo ina jumla ya majaji saba, wakati idadi kamili inayohitajika ni 15, hivyo ina upungufu wa majaji 8.
Akizungumzia kuhusu ukataji rufaa, ambapo baadhi ya wananchi walitaka kufahamu juu ya utaratibu wake,ambao ni Farida Mwalwaka mkazi wa Toangoma na Ally Idd mkazi wa Majimatitu, jijini Dar es Salaam, alisema kwamba mahakama huwawezesha wateja wake kukata rufaa kwa kuwapatia nakala za kumbukumbu zote za kesi.
Aidha Tiganga aliwataka wananchi wenye malalamiko kuhusu uendeshwaji wa kesi mbalimbali kufika katika dawati la malalamiko ambalo hufanyika siku ya Jumanne na Alhamisi kila wiki.
Kwa upande wake Hakimu Mhe. Joyce Karata, amewataka wananchi kuwa makini wakati wa utaratibu wa ukataji wa rufaa ambapo amesema kuwa rufaa inatakiwa kukatwa ndani ya muda, ili kuondoa usumbufu wa upatikanaji wa nyaraka.
0 comments:
Post a Comment