Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad amesema suala la Bunge kufikia uamuzi wa kutofanya naye kazi ni jambo zito ambalo linahitaji tathimini na kutazama athari zake.
Amesema kuwa maamuzi yakifanyika bila kuangalia athari zake yanaweza kuleta tatizo kubwa siku za baadaye.
Profesa Assad amesema hayo leo Jumatano Aprili 03, 2019 wakati akizungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa njia ya simu.
“Nafikiri ni jambo zito sana hilo na kama nilivyosema tunahitaji tathimini kali kutazama athari zake ni zipi,” amesema na kuongeza “tukifanya maamuzi ambayo hatujatazama athari zake linaweza kuwa tatizo kubwa zaidi badala ya kupata solution,”
“Mi nafikiri tukae chini tutazame, halafu tuone athari ni zipi ili kuepuka matatizo ambayo tunaweza kuyasababisha… wasiwasi wangu ni kwamba huenda linaweza likaja kuwa tatizo kubwa zaidi kuliko linavyoonekana sasa hivi.”
Profesa Assad ametoa rai kuwa hansadi ya maswali na majibu kutoka katika mahojiano yake pamoja na Kamati ya Bunge ya Maadili iwekwe wazi ili kila Mtanzania ajue nini kilichozungumzwa baada ya kuitwa na kamati hiyo.
“Rai yangu ni kwamba ile hansadi ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iwekwe wazi kwa kila mtu ili kila mtu ajue nimeulizwa kitu gani na nimejibu kitu gani,” amesema nakuongeza “ili kila Mtanzania aweze kuweka tathimini yake, halafu aweze kupima kuwa hili lilipofikiwa ni sawa au sio sawa.”
Na Emmanuel Mtengwa, Mwananchi
0 comments:
Post a Comment