Tuesday, 2 April 2019

BUNGE LAMKATAA CAG...KUMBE PROF. ASSAD ALIGOMA KUOMBA RADHI AKAKOMAA 'BUNGE DHAIFU'

...

Prof. Assad
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Prof. Mussa Assad amesema kwamba hatoacha kutumia neno dhaifu akasisitiza ataendelea kulitumia na hakujutia kulitumia dhidi ya Bunge.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maadili, Emmanuel Mwakasaka , ambaye ameeleza bungeni kwamba Kamati imejiridhisha CAG Assad amelidhalilisha Bunge na Kamati imemtia hatiani kwa kulidharau Bunge na kudhalilisha shughuli za chombo hiki.

Mbele ya Bunge, Mwakasaka ameeleza kwamba Prof. Assad alikiri mbele ya kamati kuliita Bunge dhaifu lakini alipingana na tafsiri ya neno 'dhaifu' iliyopo kwenye Kamusi ya Kiswahili Sanifu inayosema 'goigoi, hafifu, isiyo imara' akisitiza kiuhasibu udhaifu ni 'upungufu'.

Mwakasaka amesema, "tuliangalia maana ya neno upungufu kwenye kamusi tukabaini ni 'isiyo kamili, isiyo imara', hivyo alidhamiria kulidhalilisha Bunge. CAG hakuomba msamaha wala kujutia na akasisitiza ataendelea kulitumia neno hilo".

"Kamati imependekeza Bunge lisifanye kazi na CAG Prof. Mussa Assad", Mwakasaka amesisitiza.

Hata hivyo, Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe amelionya Bunge kwamba historia ambayo itaandikwa leo kuhusu CAG itawahukumu, "Bunge mnajipa utukufu ambao ni wa Mungu pekee".

"Azimio mnalotaka kulifanya leo dhidi ya CAG mmeshalifanyia kazi. Mnataka kuwanyima watu haki na uhuru wa mawazo ilhali Katiba imeruhusu kila mtu, akiwamo CAG ana uhuru wa kutoa mawazo na kueleza fikra zake, kufanya mawasiliano na kutoingiliwa kuhusu taarifa yake", ameongeza.

Utata wa kauli ya CAG ulianzia pale CAG alipokuwa akijibu swali la Mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kwamba kitendo cha ofisi yake kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonyesha kuna ubadhirifu lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea ni kutokana na 'udhaifu wa bunge'.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger