Monday 23 January 2017

Bulembo amtaka Lowassa Aachane na Siasa

...
Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo amemshangaa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kwa kuendelea kung’ang’ania siasa hadi sasa hivi, badala yake anastahili kukaa kimya kula maisha ili afaidi uzee wake vizuri.

Bulembo aliyasema hayo wakati akifunga kampeni za udiwani Kata ya Mateves iliyopo Wilaya ya Arusha juzi, ambako walitarajiwa kumchagua diwani wao katika uchaguzi mdogo. Mbunge huyo mteule wa kuteuliwa, alisema anashangaa Lowassa kung’ang’ania madaraka, badala yake anastahili kula maisha ili kufaidi uzee wake vizuri.

Alisema wapinzani wataruhusiwa kutumia barabara, maji, shule na vinginevyo, lakini kwenda Ikulu haiwezekani. 
Aidha, Bulembo alilaani kitendo cha wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuingilia msafara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliokuwa ukielekea Uwanja wa Ngorbob Sokoni kwa ajili ya kufunga kampeni za chama hicho.

Alisema wafuasi wa CCM ni wastaarabu na wavumilivu, hawakufanya fujo, bali waliwapita kwa mbele na kuelekea kwenye mkutano wa kufunga kampeni.

Mgombea Udiwani wa Kata ya Mateves, Julius Saing’ore maarufu kwa jina la Sovoyo na mgombea uenyekiti wa serikali ya kijiji, Mohamed Nassoro maarufu kwa jina la Arsenal, waliomba kura kwa wananchi hao ili walete maendeleo.

Mgombea udiwani Saing’ore aliwasihi wananchi wa kata hiyo, kumpa kura ili waliokwenda mahakamani kudai uchaguzi uliokuwa na kasoro wajue kuwa CCM ndio yenyewe.

Awali, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shabani Mdoe alisema wananchi wana imani kubwa na chama hicho na hawataki porojo, bali wanataka maendeleo.

Alisisitiza kuwa awali alipokuwa madarakani aliyekuwa diwani wa CCM kabla ya kutenguliwa na mahakama mwaka jana, Saing’ore maarufu kwa jina la Sovoyo, alifanya kazi mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama.

Alisema diwani huyo ambaye sasa anagombea tena, alikaa madarakani kwa siku 63 kama Diwani wa Kata ya Mateves kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Arusha Vijiji (Arusha DC) hivyo kurudi kwake kama diwani kutawezesha wananchi kupata maendeleo.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger