Saturday 14 January 2017

Ufafanuzi wa Wizara ya Nishati Kuhusu Tuhuma za Profesa Muhongo Kushiriki Kupandisha Bei ya Umeme

...

Wizara ya Nishati na Madini inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu kikao cha Waziri wa Nishati na Madini na Ujumbe wa Benki ya Dunia kilichofanyika tarehe 28.09.2016 kikihusishwa na kupandishwa kwa bei ya umeme kama ilivyoripotiwa na magazeti ya Mwananchi ya tarehe 12.01.2017 lenye kichwa cha habari “Prof. Muhongo alivyoshiriki kupandisha bei ya umeme” na la tarehe 13.01.2017 lenye kichwa cha habari “Prof. Muhongo awekwa mtu kati”.

Wizara inapenda kuutaarifu Umma kuwa, imekuwa ikifanya vikao na wadau mbalimbali wakiwemo Taasisi za Umma, Binafsi na Washirika wa Maendeleo yakiwemo Mashirika ya Kifedha ya Kimataifa. Lengo la vikao hivyo ni pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika Sekta za Nishati na Madini nchini.

Aidha, tarehe 28/9/2016 Wizara ilifanya kikao na Ujumbe kutoka Benki ya Dunia ikiwa ni mwendelezo wa vikao vya majadiliano kuhusu upatikanaji wa mkopo wa Dola za Marekani Milioni 200 kwa ajili ya kuboresha uendeshaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO). 
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na taasisi nyingine zikiwemo Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA).

Katika kikao hicho masuala yaliyojadiliwa yalikuwa ni;

1.  Upatikanaji wa umeme wa kutosha, uhakika na  bei nafuu kwa ajili ya kuchochea shughuli za maendeleo ya kukuza uchumi wa nchi ikiwemo viwanda, biashara, kilimo na huduma za jamii;
2.  Kuongeza ufanisi wa utendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO); na
3.  Kupunguza deni la TANESCO.

Katika kulipunguza deni la TANESCO ambalo linakaribia Shilingi Bilioni 800 (takriban Dola za Marekani Milioni 363) na kuboresha shughuli za utendaji za TANESCO, Benki ya Dunia ilijadiliana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na Madini ili kupata mkopo wa Dola za Marekani Milioni 200. Hivyo, katika kikao hicho, hakukuwa na makubaliano ya kupandisha bei ya Umeme kama ilivyoripotiwa na gazeti hilo.

Vile vile, tunaomba kuutaarifu Umma kwamba Wizara ya Nishati na Madini kwa niaba ya Serikali inafanya majadiliano na Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB), Umoja wa Ulaya (EU), JICA (Japan), na Mashirika mengine ya fedha kwa lengo la kutafuta fedha za kuboresha Sekta ya Nishati.

Imetolewa na;
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
13.01.2017
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger