Friday 20 January 2017

RATIBA YA KUHAMIA DODOMA IPO PALEPALE

...
 
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama amesema ratiba ya kuhamia Dodoma kwa mawaziri, manaibu, makatibu wakuu na manaibu iko palepale.

Amesema watakaoshindwa kufanya hivyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atatoa mwongozo. Jenista alisema jana kuwa baada ya Februari 28, mwaka huu kutafanyika tathimini na kuangalia utekelezaji wake umefikia wapi, na kwamba kwa wale ambao hawatatekeleza agizo hilo, Waziri Mkuu Majaliwa atatoa mwongozo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Jenista alisema uamuzi ulitolewa na Rais John Magufuli uko palepale.

Alisema hata Waziri Mkuu amekuwa akisisitiza ratiba ya kuhamia Dodoma kwa awamu ya kwanza Februari mwaka huu ambayo itahusisha mawaziri, manaibu mawaziri, makatibu wakuu na manaibu wao na baadhi ya watumishi wa wizara.

"Kazi yetu itakuwa ni kuangalia utekelezaji utakuwa umefikia wapi na asiyetekeleza Waziri Mkuu atatoa mwongozo,” alisema Jenista.

Pia alisema amekuwa akikagua nyumba ambazo zinafanyiwa ukarabati kwa ajili ya watumishi watakaohamia Dodoma ikiwemo nyumba za Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) eneo la Kikuyu, ambapo ukarabati wake unaendelea vizuri.

Alisema nyumba hizo za ghorofa, zitawezesha baadhi ya watumishi kupata nyumba za makazi, ambapo pia taasisi nyingine zinaendelea na ujenzi wa nyumba za watumishi.
Julai mwaka jana, Rais Magufuli alitangaza kuhusu serikali yake kuhamia Dodoma kabla ya kumalizika kwa muhula wake wa kwanza wa miaka mitano, na tayari Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikwisha kuhamia katika makao makuu hayo ya nchi yaliyotangazwa mwaka 1973.

Akiahirisha Mkutano wa Nne wa Bunge la 11 mwishoni mwaka jana, Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali itahamia Dodoma kwa awali, na kueleza kuwa awamu ya kwanza itakuwa kati ya Septemba 2016 hadi Februari, 2017 ikiwahusisha Waziri Mkuu, mawaziri, makatibu wakuu, manaibu makatibu wakuu na walau idara mbili za kila wizara.

Alisema awamu ya pili itakuwa Machi 2017 hadi Agosti 2017, ya tatu Septemba 2017- Feb 2018, ya nne Machi 2018- Agosti 2018, na ya tano Septemba 2018-Februari 2019; na kwamba awamu hizo zitatumika kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa kuhamisha watumishi hadi wote wawe wamehamia Dodoma.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger