Thursday 19 January 2017

Maiti iliyozikwa na Kisha Baadae Kukutwa Iko Nyumbani Kitandani Yazikwa Tena Chini Ya Ulinzi Mkali wa Polisi

...
Maiti ya mtoto Haruna Kyando (9) ambayo ilikutwa nyumbani muda mfupi baada ya wananchi kutoka makaburini kumzika, imezikwa kwenye makaburi ya Isanga chini ya ulinzi wa askari wa Jeshi la Polisi nchini, huku waombolezaji wakiaga mwili huo kwa kufunuliwa jeneza eneo la kichwani makaburini hapo.

Aidha, Mchungaji wa Kanisa la Bonde la Baraka, ameingizwa lawamani kwa kupotosha umma.

Haruna aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kifafa tangu udogo wake, alikutwa na wazazi wake Jailo Kyando (36) ambaye ni muosha magari na mkewe, Anna Elieza (32) akiwa amefia usingizini Jumatatu wiki hii nyumbani kwao Mtaa wa Igoma A, Kata ya Isanga jijini Mbeya.

Kilichowapa taharuki wakazi wengi jijini hapa ni baada ya ndugu, jamaa na marafiki wa familia ya Haruna walipotoka makaburini siku hiyo walikokwenda kuzika, waliporejea nyumbani waliukuta mwili wa mtoto huyo ukiwa umelazwa kwenye godoro, pale pale ulipowekwa wakati walipokuwa wakiuandaa kuuweka kwenye jeneza.

Hatua hiyo ilizua taharuki kubwa kiasi cha wananchi kutaka kufahamu ni kitu gani kilichozikwa ndani ya jeneza na ndipo Jeshi la Polisi lilipoingilia kati, kuzuia kufukuliwa kwa kaburi husika.

Hatua hiyo ilisababisha vurugu na hatimaye saa tatu za usiku siku hiyo hiyo ya maziko ya awali, Polisi wakalazimika kutumia mabomu ya machozi, kutawanya watu waliofurika katika makaburi ya Isanga wakishinikiza kaburi lifukuliwe.

Lakini juzi baada ya kukamilishwa kwa taratibu husika, ikiwemo kupatikana kwa kibali kutoka mahakamani, saa nne na nusu asubuhi, Polisi Mkoa wa Mbeya walifika eneo la makaburi alipozikwa marehemu na kusimamia shughuli nzima ya kufukua kaburi hilo.

Shughuli hiyo iliyodumu kwa muda wa nusu saa kama ilivyokuwa siku ya kwanza, ilihudhuriwa na mamia ya wakazi jijini hapa waliotaka kujua nini kilichozikwa ilhali mwili ukiwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa wakati huo.

Nusu saa baadaye jeneza la mtoto huyo lilitolewa nje ya kaburi na ndipo Mwenyekiti wa Mtaa wa Igoma A, Fredy Mwaiswelo alipofunua jeneza na kukuta ndani kukiwa tupu, hali iliyoashiria mwili wa marehemu haukuwekwa ndani ya jeneza wakati wanakwenda kuzika.

Kutokana na hali hiyo, Polisi kwa kushirikiana na baadhi ya vijana, walibeba jeneza hilo na kuelekea nalo katika Kituo cha Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi kabla ya kuwakabidhi tena wanandugu mwili ili kuendelea na taratibu za maziko kwa mara nyingine.

Baada ya ndugu kukabidhiwa mwili, jeshi hilo pia lilisimamia maziko yaliyofanyika upya saa 10 jioni katika kaburi lile lile la awali, lakini tofauti na awali, kabla ya kuzika ulifanyika utaratibu wa ndugu, jamaa na marafiki waliohudhuria, kuuaga mwili wa marehemu uliokuwa ndani ya jeneza lililofunuliwa upande wa kichwani.

Kutokana na mkanganyiko uliojitokeza, baadhi ya ndugu na majirani wa Mtaa wa Igoma, walisema tukio hilo linaweza kuwa na sura mbili kwa maana ya hujuma iliyofanywa kwa makusudi, ikilenga maslahi binafsi ya mtu inayohusishwa na imani za kishirikina au bahati mbaya ya kuusahau mwili wa marehemu.

Walisema inaweza kuwa hujuma kutokana na kawaida ya misiba kabla ya maziko, lazima ndugu watoe heshima za mwisho kwa marehemu, lakini kwa msiba huu haikufanyika pamoja na baadhi ya ndugu kutohudhuria mazishi.

Akizungumza  nyumbani kwake jana pamoja na kukanusha tuhuma za kuhusisha tukio hilo na imani za kishirikina, baba wa marehemu alisema mkanganyiko uliojitokeza wakati taratibu za kuuandaa mwili zikifanyika pamoja na uzushi uliofanywa na mchungaji, ambaye alisema hamjui kwa jina, ndiyo vilivyokuza jambo hilo.

Alisema kama ilivyo kawaida baada ya majirani kupata taarifa za msiba wakiwa nyumbani hapo, walichanga fedha na kutuma watu kwenda kununua jeneza.

“Wananchi walichanga hela wakanunua jeneza likaletwa nyumbani. Waliobeba jeneza walilisukumiza tu kwenye chumba wakatoka, sisi tukaendelea na taratibu nyingine za mazishi. Baadaye akaja mwenyekiti akasema toeni mwili wa marehemu nje, wakatoa meza nje wakatuma vijana waende kuchukua mwili wa marehemu ndani. Waliopeleka jeneza ndani na waliokwenda kulichukua ni watu wengine. Jeneza likawekwa juu ya meza tukaendelea na mahubiri,” alisema Kyando.

Alisema baadaye walikwenda kuzika na baada ya kuzika walirudi nyumbani kisha wakala chakula na kunawa maji, kama ilivyo desturi ya misiba mingi mkoani hapa.

“Tumenawa maji tukakaa. Baada ya kukaa kuna mgeni akaingia katika chumba tunacholala ambapo awali ndipo tulimlaza mtoto kwenye kigodoro, alipoweka begi akakuta kuna blanketi. 
"Alipolifunua akashtuka akasema kuna nyoka watu wakaanza kukimbia ndani. Baadhi ya watu wenye roho yenye hasira wakaamua kuingia ndani wakahakikishe kuna nini,” alisimulia. 
“Walipoingia ndani ndipo wakakuta ni mwili wa mtoto yaani marehemu. Waliposema ni mtoto wakipaza sauti watu wakajaa ndani. Ndipo waumini wa yule mchungaji wakaanza kumpigia simu yule mchungaji baadaye akarudi.”

Alisema baada ya mchungaji huyo kufika, aliingia ndani na waumini wake na kuanza kuomba.

“Walipoomba kwa muda mrefu ndipo mchungaji huyo alipotoka nje na kushika MIC na kuuambia umati kuwa mtoto baada ya kuombewa amehema mara mbili na ndipo watu wakaanza kulumbana,” alieleza.

“Kama siyo mchungaji kuzusha yale wala yasingekuzwa mpaka kwenye mitandao kiasi hiki. Sisi tunaamini walioagizwa kuchukua mwili walichukua jeneza tupu pasipo kuwekwa mwili ndani yake na kwa kuwa baada ya kutolewa jeneza hatukuingia ndani hivyo tuliuacha mwili nyumbani tukaenda kuzika jeneza peke yake,” alibainisha.

Akizungumzia suala la imani ya familia hiyo, Kyando alisema awali yeye na familia yake yenye watoto wawili, walikuwa wakisali katika Kanisa Katoliki, lakini kutokana na matatizo ya degedege yaliyokuwa yakimsumbua mwanawe wa kwanza, mkewe aliamua kumpeleka mtoto huyo kwa mchungaji wa Kanisa la Bonde la Baraka ili aombewe ikiwa ni sehemu ya kuhangaikia afya ya mtoto.

“Tulikuwa tunasali Roma, lakini kutokana na matatizo ya mtoto, mama yake akaamua aanze kusali Kanisa la Bonde la Baraka ili aombewe. Hapo mimi nikaacha kusali na ndiyo sababu hata katika ibada ya maziko ya mtoto ikabidi tulishirikishe kanisa walikokuwa wanasali mama na mtoto,” alisema Kyando na kuongeza: 
“Watu wamezungumza maneno mengi sana, siwezi kubisha japo ni ya uzushi ila wameongea kutokana na walivyosikia, ila ukweli naujua mimi na namwachia Mungu.”

Naye baba mkubwa wa marehemu, Saulo Kyando alisema jambo lililotokea lilikuwa la kawaida na kilichotokea ni kukosekana kwa uratibu makini wa msiba huo.

“Hili jambo lilikuwa la kawaida sema kilichokosekana ni mtu ambaye angeliweka jambo sawa, angekuwepo mtu wa kusimamia kila hatua yasingefikia hapa,” alisema Saulo.
Jeneza baada ya kufukuliwa kutoka kaburini
Mwenyekiti wa Mtaa wa Igoma pamoja na Baba wa Marehemu wakifunua jeneza kuhakikisha kama kulikuwa na mwili wa marehemu 
Jeneza lililofukuliwa likiwa halina kitu ndani yake 
Vijana wakiwa wanaondoa jeneza makaburini na kulipeleka kituo cha Polisi kwa ajili ya taratibu zingine
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger