Friday 27 January 2017

Tanzania na Malawi Kukutana Kujadili Sakata la Watanzania 8 Waliokamatwa

...

Tume  ya Ushirikiano wa Pamoja ya Kudumu (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi, inatarajia kukutana nchini humo kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali, ikiwemo la Watanzania nane kukamatwa nchini humo kwa tuhuma za kuingia eneo la migodini bila kuwa na kibali.

Mbali na kujadili suala la Watanzania hao, lakini pia tume hiyo itajidili mgogoro wa mpaka uliopo baina ya nchi hizo mbili katika Ziwa Nyasa.

Mkutano huo unatarajiwa kuanza Februari 3 hadi 5 mwaka huu nchini Malawi.

Akizungumza Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga alisema tume hiyo ilikuwa haijakutana kwa muda mrefu, jambo ambalo limesababisha watu kuwa na sintofahamu kati ya ushirikiano wa nchi hizo mbili.

Kasiga alisema mkutano wa tume hiyo, mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2003 jijini Dar es Salaam, hivyo kuwa kimya kwa muda mrefu kuna baadhi ya watu walidhani kuwa ushirikiano wa nchi hizo mbili si mzuri.

“Kikao kama hiki kilikaa miaka mingi kidogo… kuna masuala yaliyochelewa kutekelezwa kutokana na kukaa kwa kikao hiki, lakini kwa sasa yatatekelezwa kupitia vikao hivyo,” alisema Kasiga.

Aliongeza kuwa kwa mara ya kwanza, vikao hivyo vitashirikisha wafanyabiashara kutoka mikoa ya Njombe na Ruvuma, pia wavuvi kutoka katika mikoa hiyo ambao wataeleza namna wanavyofanya shughuli zao kwa kushirikiana na wenzao wa Malawi bila kuingilia.

Mindi alisema katika kikao hicho, ujumbe wa Tanzania utaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga; na mbali na kujadili mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa na Watanzania waliokamatwa, pia utajadili masuala mbalimbali katika sekta za biashara, elimu, kilimo pamoja na sekta zingine.

Kasiga pia alikabidhi tuzo za Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) walizoshinda kutoka Umoja wa Afrika (AU). SSRA ambayo imekuwa wa kwanza katika Tuzo za Ubunifu Katika Sekta za Umma Afrika (AAPSIA), ilikabidhiwa kikombe pamoja na cheti cha ushindi.

Ushindi huo wameupata kupitia mradi wao wa Mradi wa Kanzidata ya Taifa ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii.
Bi Mindi akimkabidhi Bi. Sarah kombe la ushindi kwa niaba ya Wizara. Bi. Kibonde aliipokea zawadi hiyo kwa niaba ya Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Meneja wa Mradi wa Mfumo wa Forodha wa TANCIS kutoka TRA akipokea zawadi ya cheti cha ushindi kutoka kwa Bi. Mindi Kasiga.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger