Friday, 6 November 2020

WANARIADHA 500 KUCHUANA KATIKA MBIO ZA KAHAMA MARATHON 2020 JUMAPILI HII

...

 Waandaaji wa mashindano ya Kahama Marathon Season One 2020 wakionesha jezi zitakazotumika kwenye mbio hizo Novemba 8, mwaka huu mjini Kahama

Mmoja wa waandaaji wa Kahama Marathon Season One 2020, Caroline Joseph akizungumzia maandalizi ya mbio hizo
Afisa Michezo Halmashauri ya Mji wa Kahama, Rupolwa Mkomwa akielezea namna mji huo utakavyonufaika na mashindano hayo 
Mratibu wa Kahama Maratahon Season one 2020, Siya Kimambo amewaomba wadau wengine kujitokeza kusapoti mashindano hayo, huku akiwashukuru wadau mbalimbali waliosaidia kufanikisha mbio hizo wakiwemo Jambo Group, TBL, Keke Bridal, Stockholm Car Wash, Rocken Hill Schools, Zengo Bar and Grill, Jema Africa na Emirates Alluminium.
Mmoja wa wadhamini wa mbio hizo, Mayalla Moses ambaye ni Meneja wa Zengo Bar & Grill iliyopo mjini Kahama akiwakaribisha wadau mbaimbali kwenye mbio hizo
Mmoja wa washiriki wa mbio za Km 21, Allan Kabasere akizungumzia namna alivyojiandaa kufanya vizuri kwenye mashindano ya Kahama Marathon Season one 2020
JUMLA ya wanariadha 500 kutoka mikoa mbalimbali nchini wanatarajia kushiriki mbio za Kahama Marathon Season One 2020 zitakazofanyika Novemba 8, mwaka huu wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga. 

Wanariadha watachuana kwenye mbio za Kilometa 21, 10 na tano zitakazoshirikisha pia watoto, wazee na wagonjwa, zikiwa zimebeba kaulimbiu ya ‘Okoa vifo vya mama wajawazito na watoto’ ambapo sehemu ya kiasi cha fedha zitakazopatikana kwenye mashindano hayo zitapelekwa kwenye hospitali kuwasaidia wamama wajawazito na watoto. 

Akizungumzia maandalizi ya mashindano hayo, mmoja kati ya waandaaji wa Kahama Marathon, Calorine Joseph amesema kuwa huu ni msimu wa kwanza wa mbio hizo ambapo tayari zoezi la uandikishwaji limefunguliwa na tayari washiriki 350 wamekwishajiandikisha, huku wakitarajia kupata wakimbiaji 500. 

“Kilele cha mbio hizi ni Jumapili hii na tunawaalika wadau wote wa michezo waje wajiandikishe kwa ajili ya kushiriki, watu wajitokeze kwa wingi tunataka kuitangaza Kahama na kuuinua kwenye michezo kupitia mbio hizi, pia kuutangaza mji huu kifursa, kiuchumi na kiutamaduni. 

“Kwakuwa ndiyo tunaanza basi wajiandikishe kwa wingi, tunaamini mwakani mambo yataboreshwa zaidi na zawadi zitaongezeka, mpaka sasa washiriki 350 wameshajitokeza, na matarajio yetu ni kufikisha washiriki 500 ambao wametoka sehemu mbalimbali ikiwemo Mwanza, Singida, Mbeya, Dar es Salaam, Arusha, Kahama, Musoma na Geita…tunakoelekea misimu ijayo kwenye mbio hizi ni kufika washiriki 1,000,” amesema. 

Amesema kuwa washiriki watachuana kwenye mbio zenye urefu wa Kilometa 21 na 10, huku wazee, watoto na wagonjwa wakikimbia mbio za kilometa tano, ambapo mshindi wa kwanza kwa Km 21 kwa wanaume na wanawake watapata Sh 400,000, washindi wa pili Sh 300,000 na Sh 200,000 kwa washindi wa tatu. 

Kwa upande wa mbio za Kilometa 10, washindi wa kwanza watapata Sh 300,000, washindi wa pili Sh 200,000 na wa tatu Sh 100,000, huku Km tano kwa upande wa watoto wakitarajia kutoa zawadi ya Sh 30,000 kwa mshindi wa kwanza, Sh 20,000 kwa mshindi wa pili na Sh 15,000 kwa washindi wa tatu. 

Amebainisha kuwa washiriki wa mbio za Km 21 na 10 watajiandikisha kwa kiingilio cha Sh 30,000 huku watoto wakijiandikisha kwa Sh 25,000, ambapo washiriki wote watakaojisajili baada ya kulipa kiingilio watapata fulana, namba na medali. 

Kwa upande wake, Afisa Michezo wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Rupola Mkomwa , amewashukuru waandaaji wa mbio hizo kwa kuona umuhimu wa kuleta mashindano hayo wilayani kahama, kwani ni moja ya njia ya kuutambulisha mji huo na kuwafanya wadau watambue kwamba Novemba 8 kuna jambo litafanyika Kahama. 

“Wadau hawa wamefanya kazi ya serikali na ya chama cha riadha, na kama kuna wadau wangependa kujitokeza kuwaunga mkono ili kila mwaka tufanikishe jambo hili basi wajitokeze kwa sababu wamesaidia vijana kupata wenye vipaji kupata ajira….Naomba tuwaunge mkono waandaji hawa kwa sababu wanalenga pia kuisaidia jamii ya kitanzania wakiwemo watoto na akina mama wajawazito,” alisema. 

Mmoja wa washiriki wa mbio hizo, Allan Kabasere, ambaye amejiandikisha kukimbio mbio za Km 21, amewashauri vijana wenzake kujitokeza, huku akieleza kuwa ameshawishika baada ya kuvutiwa na nia ya waandaaji hao katika kusaidia watoto na wanawake, ambapo amejinadi kuwa atashinda mbio hizo kwani amekuwa na uzoefu tangu akiwa shuleni. 

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger