Wednesday, 25 November 2020

Halima Mdee na Wenzake Waitwa Kujieleza CHADEMA

...


Katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika amesisitiza kuwa chama hicho hakikufanya uteuzi wa wanachama wao 19 ambao jana Jumanne Novemba 24, 2020 waliapishwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kuwa wabunge wa viti maalum.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Novemba 25, 2020, Mnyika amesema chama hicho hakijateua wabunge hao wala kupeleka orodha ya majina Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), huku akitoa wito wa kuwataka wabunge hao kufika katika ofisi za chama hicho  keshokutwa Ijumaa, Novemba 27, ili kuhojiwa na Kamati Kuu ya Chama kutokana na kitendo walichokifanya.

“Tumewaita kuwaeleza kwamba Chadema hakijateua wabunge wa viti maalum wala hakijawasilisha orodha yoyote Tume Uchaguzi ya uteuzi wa wabunge wa viti maalum. Kwa katiba ya Chadema mamlaka ya uteuzi wa wabunge yako kwa kamati kuu ya chama, na kamati kuu ya chama haijawahi kufanya kikao cha uteuzi wa majina ya wabunge wa viti maalum na mimi Katibu Mkuu sijawahi kuwasilisha orodha yoyote Tume ya Uchaguzi.

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilituandikia barua Novemba 10, 2020 kutueleza haijapokea majina ya wabunge wa viti maalum na kutuomba kuyawasilisha ikiwemo fomu namba 8D inayopaswa kuwa na idhini ya katibu mkuu wa chama na mimi sijajaza yoyote. Niliiandika baada ya Mkurugenzi wa NEC kunukuliwa na vyombo vya habari kwamba Chadema imewasilisha orodha ya wabunge wa viti maalum na yeye amekwishaipeleka bungeni.

“Mimi kama Katibu Mkuu hakuna fomu yoyote niliyowahi kuijaza popote kuthibitisha uteuzi wa yeyote, hii fomu pia ina sehemu ya kiapo cha hakimu, kwa tafsiri nyepesi kilichofanyika ni  kughushi na wameenda kuapishwa bila baraka ya chama.

“Tumeitisha kikao cha kamati kuu Ijumaa, Novemba 27, 2020, Dar es Salaam, na tutawaandikia wahusika ili kisitokee kisingizio hakupata taarifa, natangaza wito kwa wanachama wetu 19 walioshiriki kuapishwa kufika makao makuu Kinondoni Ijumaa saa 2:00 asubuhi,” alisema Mnyika.

Aidha, amesema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ataongoza kikao cha kuwahoji wanachama walioapishwa kuwa wabunge wa viti maalum akiongeza kwamba si mara ya kwanza wao kufanya vikao vya kinidhamu na walioapishwa wameshiriki kukihujumu chama.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger