Wazalishaji na wasindikaji wa Mafuta ya Kula Mkoani Kigoma wametakiwa kufuata kanuni za uzalishaji bora ili kuweza kukuza biashara ya Mafuta ya kula nchini.
Ameyasema hayo hivi karibuni Meneja Mafunzo na Utafiti wa TBS, Bw. Hamis Sudi katika kata ya Mkongoro wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wasindikaji wa mafuta ya mawese yanayoendelea mkoani Kigoma. Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Halmashauri ya wilaya ya Kigoma yalihudhuriwa na washiriki wapatao 200 kutoka kata za Mkongoro na Bitale.
Akizungumza katika mafunzo hayo Bw.Sudi amesema mzalishaji ili aweze kukuza biashara yake ya mafuta inamlazimu kufuata kanuni za uzalishaji bora ili kuweza kupata masoko ya uhakika.
"Mnapaswa kufuata kanuni za uzalishaji bora kwa maana hiyo mtakuwa mmeiongezea thamani bidhaa zenu na kuwawezesha kuzalisha kwa wingi na kupata masoko mengi". Amesema Bw.Sudi.
Aidha Bw.Sudi amewaomba wazalishaji kutumia fursa ya mafunzo wanayoyapata Wazalishaji hao kwa kuwauliza maswali maafisa wa Serikali ili kuweza kutatuliwa matatizo yanayowakabili katika uzalishaji wa mafuta ya kula.
Pamoja na hayo Bw.Sudi amesema iwapo wazalishaji na wasindikaji wa mafuta wakiyatumia vizuri mafunzo hayo wanayoyapata wataweza kukuza biashara yao ya mafuta.
0 comments:
Post a Comment