Dar es Salaam Tanzania, 25 Novemba 2020 - Benki ya Azania ikiwa katika maadhimisho ya kusherehekea miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, maadhimisho ambayo imeyaita “Mwaka wa Kifaru” kuonesha uimara wa benki hiyo kwenye soko,leo hii imezindua huduma mpya ya kisasa ya kadi za VISA kwa wateja wake.
Kadi hizo ambazo ni za aina mbili, yaani kadi za kawaida (Classic) na zile ya daraja la juu (Infinite) ambazo itatumiwa na wateja wake wa akaunti maalum, zimezinduliwa katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika ofisi za Benki hiyo zilizopo Obama Drive, Sea View- Upanga jijini Dar es salaam. Kwa kutumia Kadi hizo mbili sasa wateja wa Benki hiyo wataweza kufanya miamala popote duniani na kuweza kufanya manunuzi kwa njia ya mtandao, kufanya malipo kwa kutumia kadi hizo za Visa kwenye maduka mbalimbali nk. Wateja wa kadi za daraja la juu (Infinite card) wataweza kupata huduma za ziada ikiwamo huduma katika viwanja vya ndege, hoteli za kimataifa na kadhalika.
Akiongea wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo Bw. Charles Itembe iliishukuru bodi ya Benki hiyo kwa kuwaunga mkono katika kufanikisha safari ya Benki hiyo yenye lengo la kuifanya Benki izidi kuwa ya kisasa zaidi.
“Ikumbukwe kuwa kipindi hiki tuko katika maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Benki yetu mwaka 1995. Kwa kuwajali wateja wetu kwa kutuunga mkono kwa miaka 25 tumehakikikisha wateja wetu wanaendelea kufurahia huduma zetu zote zikiwamo za kubenki kidijitali, kwa kutumia simu zao za kiganjani kwa mobile App iliyoboreshwa, Mawakala wetu ambao wamesambaa nchi nzima, matawi yetu ambayo sasa yamefikia 24 ambapo baadhi yanatoa huduma 8-8, siku zote 7 za wiki, vituo vyetu vya kutolea huduma (Service Centres), Maduka ya kubadilishia fedha yanayojitegemea 12, na mwishoni mwa wiki hii pia tunakwenda kufungua duka jingine la 13 katika uwanja mpya wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA Terminal III), na huduma nyinginezo nyingi na za kipekee kabisa. Na sasa tumewaletea huduma hii kubwa kabisa ya kadi za VISA”, aliongeza Bw.Itembe.
“Benki yetu imewekeza katika teknolojia ya kisasa, mfumo wetu wa teknolojia ya kibenki wa Oracle Flexcube toleo la 12.4 ni wa kisasa zaidi na ndio uliotuwezesha kutuunganisha na huduma hii ya VISA inayopatikana dunia nzima na wateja wetu sasa wataweza kupata huduma kwa kutumia kadi zao za VISA popote duniani” alimalizia Bw.Itembe.
Naye Meneja wa huduma za Benki Kidijitali wa Benki hiyo Bw. Vinesh Davda aliongezea kuwa huduma hii itawapa urahisi wateja wa Benki na hivyo aliwaomba wateja wao watembelee matawi ya benki hiyo ili kuweza kupata kadi hizo mpya.
0 comments:
Post a Comment