Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) leo Ijumaa tarehe 27 Novemba 2020, kinafanya kikao maalum cha kamati kuu kuwajadili wanachama wake 19 wanaodaiwa kukisaliti kwa kukubali uteuzi wa ubunge viti maalumu.
Kikao hicho, kinafanyika jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.
Wanachama hao 19 wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee wanajadiliwa baada ya tarehe 24 Novemba 2020 kwenda bungeni jijini Dodoma kuapishwa na Spika Job Ndugai.
Kufuatia hali hiyo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alitangaza kufanyika kwa kamati kuu leo Ijumaa na kuwataka kufika makao makuu ya Chadema, Kinondoni Dar es Salaam saa 2:00 asubuhi.
Hata hivyo baadhi ya wanachama wa Chadema wakiwemo wajumbe wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha) wakiwa nje ya ofisi za makao makuu mtaa wa Ufipa, Dar es Salaam na mabango wakishinikiza chama hicho kuwafukuza uanachama makada 19 wa chama hicho ambao wameapishwa kuwa wabunge wa Viti Maalum mjini Dodoma bila idhini ya Chadema.
0 comments:
Post a Comment