Serikali ya Somalia imesema kuwa imemuita nyumbani balozi wake nchini Kenya Mohamud Ahmed Nur Tarzan, na kuishutumu nchi hiyo kwa kuingilia siasa za nchi yake.
Somalia pia imemtaka balozi wa Kenya nchini Somalia kufunga virago "kwa ajili ya majadiliano".
Somalia imeishutumu Kenya kwa kushinikiza serikali ya Jubbaland kukataa makubaliano ya uchaguzi yaliofikiwa Septemba 17, katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika mwezi ujao.
"Serikali ya Somalia ilichukua uamuzi huo kulinda eneo lake la utawala baada ya kujitokeza kuwa Kenya inaingilia kimaksudi masuala ya Somalia eneo la Jubbaland," Mohamed Ali Nur, Waziri wa mambo ya nje wa Somalia amesema katika taarifa iliyotolewa.
"Serikali] ya Somalia imeonesha kusikitishwa kwake na serikali ya Kenya kwa kuingilia moja kwa moja masuala ya ndani ya siasa za Somalia hatua ambayo inaweza kuchangia ukosefu wa uthabiti, usalama na maendeleo kwa eneo zima,” taarifa hiyo imesema.
Kenya inaunga mkono utawala wa Ahmed Mohamed Islam maarufu kama "Madobe" huko Jubbaland, kwasababu ya maslahi yake ya kiusalama na kieneo.
-BBC
0 comments:
Post a Comment