Thursday, 26 November 2020

WANAUSHIRIKA KIGOMA WATAKIWA KUTUMIA FURSA YA KILIMO CHA MICHIKICHI

...
 Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Charles Malunde, amewataka Viongozi wa Vyama vya Ushirika vinavyolima zao la Michikichi mkoani Kigoma kushirikiana kwa pamoja ili kuongeza nguvu ya kuzalisha na kukuza miche bora ya Chikichi kwenye vitalu ili wakulima wapate miche hiyo kwa wakati pale inapohitajika.

Bwana Malunde ametoa wito huo  Jumanne, Novemba 24, 2020 mjini Kigoma alipokutana na viongozi wa Vyama vya Ushirika vinavyolima zao la Michikichi ambapo amewataka kushirikiana Serikali katika kuongeza uzalishaji wa michikichi mkoani humo.

“Wanaushirika na Wanakigoma kwa ujumla itumieni fursa hii ya kilimo cha zao la Michikichi kwa kuwa ardhi mnayo na inayofaa kwa kilimo hiki, mkizembea msishangae watu kutoka maeneo mengine wakachangamkia fursa hii na kuanzisha mashamba makubwa nakumiliki soko,” amesema Naibu Mrajis.

Aidha, Bw. Malunde amesema kuwa Viongozi wa Vyama vya Ushirika watakaoshindwa kuwahamasisha na kuwashirikisha wanaushirika na wakulima kwa ujumla kuzalisha na kukuza miche bora ya Chikichi, wajipime na kuona kama bado wanafaa kuchaguliwa kuendelea kuviongoza vyama hivyo.

“Kama kiongozi ameshindwa kuwahimiza wanachama wake kushiriki katika kazi za kujiletea maendeleo; ikiwemo kuongeza uzalishaji wa mazao yao, hatuoni sababu za yeye kuendelea kukiongoza chama cha ushirika,” amesema Naibu Mrajis.

Taarifa iliyotolewa na Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Kigoma, Robert Kitambo, wakati wa ziara ya Naibu Mrajis imeonesha kuwa eneo lililopandwa Michikichi mkoani Kigoma ni Hekta 19,656 na eneo linalofaa kwa ajili ya kupanua kilimo cha Chikichi ni Hekta 48,085.

“Jumla ya eneo linalofaa kwa kilimo cha Chikichi ni Hekta 67,880 ambapo eneo hilo kwa ujumla wake linahitaji miche 9,503,340 kuikidhi eneo lote linalofaa kwa kilimo cha michikichi. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kupitia Sekretarieti ya Mkoa inaendelea kuhimiza na kusimamia ufufuaji wa zao la michikichi kupitia Taasisi za Serikali zilizopo mkoani Kigoma na Wadau mbalimbali kutoka Sekta Binafsi,” amesema Kitambo.

Mkoa wa Kigoma baada ya kutolewa kwa Agizo la Serikali la kufufua kilimo cha Chikichi mwaka 2018, vyama 13 vya ushirika vimeanzishwa na kusajiliwa: Luiche Basin AMCOS, Kasuku AMCOS, Simbo AMCOS, Mahembe AMCOS, Chakulu AMCOS, Bitale Mkongoro AMCOS, Nkungwe AMCOS, Mkuti Mchikichi AMCOS, Kagongo AMCOS, Mungonya AMCOS, Ngogomyi AMCOS, Wamiki AMCOS na Wami AMCOS.


 


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger