WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza waendesha maghala kuacha kukata tozo ya upungufu wa uzito wa korosho ghafi zilizohifadhiwa ghalani (unyaufu) kwa wakulima na wanunuzi kwa kuwa tozo hiyo imeshaondolewa na suala hilo halijathibitishwa kitaalamu.
Ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Novemba 28, 2020) katika kikao kati yake na Wakuu wa Mikoa ya Pwani, Lindi, Mtwara na Ruvuma, Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Kilimo, Viwanda na Biashara pamoja Mrajisi wa Ushirika.
Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Korosho, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maghala na Waendesha Maghala wote wa mikoa hiyo. Kikao kilifanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma.
“Mimi niliwaita kuwaambia kuwa wasimamizi wa maghala hampaswi kukata tozo ya unyaufu iwe ni kwa wakulima au wanunuzi kwasababu tozo hii haina uhalisia na haijathibitishwa na na vyombo husika, hakuna unyaufu unaotokea katika kipindi kifupi cha kuhifadhi korosho, hayo yote ni mawazo yenu tu”,”Amesema.
Waziri Mkuu amesema “Hizi Korosho wala hazikai miezi mitatu (3) kama ilivyoelekezwa kwenye kanuni hii, korosho zinazoanza mwezi wa kumi mnada unaanza mwezi wa kumi uleule na baada ya hapo kuna minada ya kila wiki, minada ipo mingi, korosho hazikai kutoka siku zinaanguka na kuokotwa mpaka kwenda kuuzwa, unyaufu mnaoukata unatokana na nini?”.
Hivyo, Waziri Mkuu amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara kumuondoa katika nafasi yake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maghala Bw. Odilo Majengo kwa kushindwa kutekeleza maagizo ya Serikali kuhusu kusitisha tozo ya unyaufu katika zao la korosho.
“Mkurugenzi wa Bodi ya Maghala ulidharau maagizo ya Serikali na hatuwezi kuishi hivyo katika Serikali, tulikwambia uache lakini ukaendesha zoezi hili kwa sirisiri na unasema hayo ni matamko ya kisiasa, kwanini tubaki na wewe kwenye nafasi hiyi”.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa siku tano kwa waendesha maghala kuandaa taarifa kuhusu ni kiasi gani cha korosho ambazo wamechukua kutoka kwa wanunuzi kama tozo ya unyafu, hivyo atatuma timu maalum kwa ajili ya kazi hiyo.
“Na ninyi waendesha maghala naleta timu huko kuja kupita kila ghala kuona msimu huu wote mmechukua korosho za unyaufu kiasi gani, kwahiyo nawapa siku tano kila mmoja akaandae taarifa ya korosho zilizochukuliwa kutokana na unyaufu katika ghala lake, kwa maghala yaliyopo mikoa ya Pwani, Lindi, Mtwara na Ruvuma kuona nani amechukua unyaufu na kwa kiasi gani”.
0 comments:
Post a Comment