Na Suzy Luhende, Shinyanga
BAADHI ya Viongozi wa dini mkoani Shinyanga wametoa msimamo wao juu ya kinachoendelea nchini baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika Oktoba 28, mwaka huu, huku baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kutoka upinzani wakihamasisha Watanzania kuandamana kwa kile kinachotajwa kupinga matokeo ya uchaguzi huo yaliyompa ushindi Rais Dk. John Magufuli.
Wakizungumza na Shinyanga Press Club Blog kwa nyakati tofauti mjini Shinyanga, viongozi hao wamesisitiza amani na umoja katika kipindi hiki, huku wakieleza kwamba maandamano yanayoitishwa na vyama vya siasa siyo sahihi kwani ni kuchochea vurugu na kuwagawa Watanzania.
Mmoja wa viongozi hao, Askofu wa Kanisa la Evangelical Assembiles of God Tanzania (EAGT) Kanda ya Kagera, Geita, na Shinyanga, Raphael Machimu ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya amani mkoa wa Shinyanga amesema, tamko lililotolewa na viongozi wa siasa la kuandamana sio sahihi wanatakiwa wafuate kanuni na sheria ya tume ya uchaguzi.
Askofu Machimu ambaye anachunga kanisa la EAGT lililoko Tambukareli manispaa ya Shinyanga ameyasema hayo Novemba 1, 2020 ofisini kwake, ambapo amesema utaratibu unaotaka kuchukuliwa sio sahihi kwa sababu hata kama wameona kuna mambo hayakuenda sawa yalitakiwa yafuatiliwe kisheria na kikatiba.
Amesema kuhamasisha watu watoke barabarani ni kitendo kibaya kinachoweza kusababisha vurugu ambayo haitakuwa na majibu, tume ya uchaguzi ambayo ina miongozo yake ambapo walitakiwa kwenda kusaidiwa huko.
"Watu wakitoka barabarani kuandamana wataumia hata watu wengine wasiohusika, mimi mwenyewe kama kiongozi naona utaratibu unaotaka kuchukuliwa sio sahihi kwa sababu hata kama wameona kuna mambo hayakuenda sawa yalitakiwa yafuatiliwe kisheria na kikatiba sio kuandamana "amesema Machimu.
Amesema tangu kuanza kwa mchakato wa uchaguzi yeye kama katibu wa amani pamoja na viongozi wenzake wamekuwa wakiomba ili Mungu ahusike kuwapa viongozi watakaoongoza vizuri na kufanya maendeleo katika kata, majimboni na ngazi ya Urais ikiwa ni pamoja na kudumisha amani.
"Katika vikao vyetu vyote tulikubaliana kuelimisha watu katika kudumisha amani kwa watu wote, na tumewaelimisha wachungaji mashehe wawaelimishe waumini wao ili kulinda amani ya Tanzania"amesema Machimu.
"Tunatakiwa tuliombee Taifa letu kwa ajili ya kudumisha amani na utulivu watu wasijiingize kwenye mkumbo wa mafarakano, sisi kazi yetu kanisa ni kuomba,yeyote atakayepita ni diwani wetu, ni mbunge wetu na ni Rais wetu awe mkristo awe muislamu"ameongeza.
Naye Askofu wa Kanisa la Philadelphia Miracle Temple lililopo Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, Baraka Laizer aliwaomba waumini wake waendelee kuliombea Taifa na waendelee kuwa watulivu wasijiingize kwenye mikusanyiko isiyokuwa ya amani badala yake wadumishe amani na upendo.
"Namshukuru Mungu kwa sababu tumekutana tena tukiwa wazima, kama nilivyowaasa kwamba msijihusishe kwenye mambo ambayo yatasababisha vurugu badala yake tuwe watulivu, kweli mmekuwa watulivu na sasa tuendelee kutulia katika nyakati hizi tusijichanganye tukajiingiza kwenye makundi ya kuvuruga amani tuendelee kuomba ili amani yetu iendelee kuwepo"amesema Laizer.
CHANZO - SHINYANGA PRESS CLUB BLOG
0 comments:
Post a Comment