Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Debora Magiligimba
Na Marco Maduhu- Shinyanga.
Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, limewaonya viongozi wa vyama vya siasa pamoja na wafuasi wao, wasijaribu kufanya maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu ,bali waende mahakamani kupinga matokeo hayo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Debora Magiligimba ametoa onyo hilo leo Jumapili Novemba 1,2020 wakati akizungumza na waaandishi wa habari.
Amesema kuwa kuna matamko yametolewa na viongozi wa kisiasa kutaka kufanya maandamano yasiyo na kikomo nchi nzima na kuanzia kesho ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu.
Kamanda Magiligimba amesema maandamano hayo ni batili, ambapo viongozi hao walipaswa kufuata sheria kwa kupinga matokeo hayo mahakamani, na siyo kufanya maandamano ambayo yana viashiria vya uvunjifu wa amani.
"Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga halitasita kamwe kuchukua hatua kali za kisheria, kwa kikundi chochote kile cha kisiasa chenye nia ya kuvuruga amani ya nchi," amesema Magiligimba.
"Kama wagombea hawajaridhika na matokeo ya uchaguzi mkuu wafuate sheria ,kanuni, na taratibu za nchi na kupeleka malalamiko yao Mahakamani na siyo kufanya maandamano ya bila kikomo yenye viashiria ya uvunjifu wa amani," ameongeza.
Pia amewataka wananchi wa mkoa wa Shinyanga kutojiingiza kwenye maandamano hayo, bali waendelee na shughuli zao za kila siku za kujiingizia kipato ,na wasiwe na hofu ikiwa ulinzi utaimarishwa kila kona.
Katika hatua nyingine amewaomba viongozi wa dini, kuendelea kusisitiza umuhimu wa amani kwa waumini wao,ili kuendelea kuilinda amani ya nchi iliyopo hivi sasa.
0 comments:
Post a Comment