Saturday, 14 November 2020

NI MARUFUKU KULISHA MIFUGO VYAKULA VIBOVU-SERIKALI

...
Mkurugenzi wa Uendelezaji Malisho na rasilimali za vyakula vya Mifugo Dkt. Asimwe Rwiguza (kulia) akifafanua jambo mbele ya wataalam wa ukaguzi wa malisho na rasilimali za vyakula vya mifugo muda mfupi baada ya kufika kwenye kiwanda cha kusindika chakula cha mifugo kinachojulikana kama "Musoma Animal Feed" kilichopo mkoani Mwanza leo
Meneja wa Kiwanda cha "Musoma Animal Feed" Bi. Maajabu Musa (mwenye kilemba cheusi) akitoa maelekezo ya namna chakula cha mifugo kinavyotengenezwa kiwandani hapo mbele ya timu ya wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wakaguzi wa vyakula vya Mifugo kutoka Mikoa ya Mwanza, Arusha, Shinyanga na Arusha wakati wa ziara yao waliyoifanya leo (13.11.2020) mkoani Mwanza.
...........................................................................................
Serikali imepiga marufuku matumizi ya vyakula vilivyopoteza ubora wa kutumiwa na binadamu na kutumiwa kama vyakula vya mifugo kabla ya kuthibitishwa kwanza na wataalam wa maabara ya mifugo.
Hayo yamesemwa leo (13.11.2020) na Mkurugenzi wa Uendelezaji Malisho na rasilimali za vyakula vya Mifugo Dkt. Asimwe Rwiguza ikiwa ni sehemu ya kuhitimisha mafunzo ya siku mbili ya wakaguzi wa vyakula vya mifugo kutoka mikoa ya Mwanza,Shinyanga, Singida na yaliyofanyika Mkoani Mwanza.
"Kumekuwa na mazoea ya vyakula ambavyo vimeshapoteza ubora wa matumizi ya binadamu kutumika kama vyakula vya mifugo hivyo ninapenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa wafugaji, wazalishaji na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na uzalishaji wa vyakula vya binadamu kuwa ni marufuku kutumia vyakula hivyo bila Wizara yenye dhamana kuwa na taarifa na kujiridhisha kitaalam kama chakula hicho kinafaa au la" Amesisitiza Dkt. Rwiguza.
Aidha Dkt. Rwiguza amebainisha madhara yanayoweza kumpata mtu ambaye atatumia mazao ya mfugo uliokula vyakula hivyo kuwa ni pamoja na kupatwa na magonjwa mbalimbali kama vile Kansa.
Upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji Malisho na rasilimali za vyakula vya Mifugo Bw. Roggers Shengoto amesema kuwa mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa sababu sehemu zaidi ya asilimia 90 ya wataalam walioalikwa walishiriki.
"Pia kupitia mafunzo haya tumegundua kuwa bado kuna haja ya Halmashauri za vijiji kutenga maeneo ya malisho ya mifugo na pia wazalishaji na wauzaji wa vyakula vya mifugo bado hawazingatii sheria na kanuni za kufanya shughuli hizo hivyo tuna imani wataalam hawa wataenda kuleta mabadiliko katika maeneo yote yenye changamoto kwa mfugaji" Ameongeza Shengoto.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema kuwa wamenufaika na yote waliyofundishwa ambapo wameahidi kuyafanyia kazi na kubadilisha utendaji wao pindi wakirejea kwenye vituo vyao vya kazi.
"Kwa mfano, zamani nilikuwa naenda kwa mdau kama Mkaguzi na nilikuwa natumia lugha ya mamlaka lakini kupitia mafunzo haya nimefundishwa kumfuata mdau kama rafiki na kuzungumza naye kwa lugha ya kawaida" Amesema mmoja wa washiriki Veronica Ngoso.
Takribani wakaguzi 129 nchi nzima wanatarajiwa kupatiwa mafunzo hayo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kufuata taratibu, sheria na kanuni.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger