Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo, CPA Nicodemus Mkama akizundua mfumo wa kuuza na kununua hisa kwa njia ya simu za mkononi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam leo jijini Dar Es Salaam.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo, CPA Nicodemus Mkama akizungumza mbele ya Wageni waaalikwa wakati wa kuzindua mfumo wa kuuza na kununua hisa kwa njia ya simu za mkononi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam leo jijini Dar Es Salaam.
Baadhi ya Wageni waalikwa mbalimbali wakifuatilia yaliyokuwa yakijiri wakati wa uzinduzi huo leo jijini Dar es salaam
Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA)imezindua mfumo wa kuuza na kununua hisa kwa njia ya simu za mkononi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam huku ikiwataka watanzania wote waliopo ndani na nje ya nchi kutumia mfumo huo mpya kwani sasa huduma imeletwa mikononi mwetu kupitia Hisa Kiganjani.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mfumo huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo, CPA Nicodemus Mkama amesema mfumo wa hisa kiganjani ni matokeo chanya ya ushirikiano wa wadau katika sekta ya masoko ya mitaji, wenye lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi madhubuti wa Rais John Magufuli kuhakikisha wanawezesha wananchi wetu kiuchumi kwa kuwafikishia huduma popote walipo, mijini na vijijini, hivyo kuinua vipato vyao hususani wananchi wenye kipato cha chini.
Aidha mfumo huu ni matokeo ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) yenye lengo la kufikisha huduma kwa wanchi wengi zaidi hususani wa kipato cha chini walio vijijini ambapo huduma hii hapo awali ilikuwa haipatikani.
Amesema hatua hiyo ni muhimu kwani inatarajia kuongeza idadi ya wawekezaji katika masoko ya mitaji na kuchangia utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Huduma za Kifedha hapa nchini yaani National Financial Inclusion Framework.
"Ninayo furaha kutamka mfumo wa uuzaji hisa kwa kutumia simu za mkononi umeidhinishwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana baada ya kukidhi matakwa ya kisheria, vigezo na kanuni za usimamizi wa masoko ya mitaji ikiwa ni pamoja na kanuni za usimamizi wa masoko ya mitaji kimataifa zinazotolewa na Taasisi ya Usimamizi wa Masoko ya Mitaji Ulimwenguni yaani International Organisation for Securities Commission (IOSCO).
"Kwa mantiki hiyo, napenda kutumia fursa hii kuipongeza Bodi na Menejiment ya Soko la Hisa la Dar es Salaam kwa kufanikisha shughuli za uundwaji wa mfumo huu. Nawapongeza pia wote waliohusika katika kufanikisha uundwaji wa mfumo huu ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Idara ya Malipo Mtando (GePG), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Taaasi ya Kuendeleza Sekta ya Fedha (FSDT), Kampuni ya MagillaTech, Benki washirika na Kampuni za Simu, na wengine wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine,"amesema.
Ameongeza uwepo wa Mfumo wa Kuuza na Kununua Hisa kwa Kutumia Simu za Mkononi unatarajiwa kuleta matokeo chanya katika kujenga Sekta Jumuishi ya Fedha. Kwa mujibu wa utafiti wa Finscope Tanzania wa mwaka 2017, zaidi ya asilimia 60 ya watu wazima wanatumia huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi.
Aidha amesema kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) za kipindi cha robo mwaka kilichoishia Septemba 2020, idadi ya watanzania wanaotumia simu za mkononi ni milioni 49.2 na watanzania wanaotumia huduma za fedha kwa njia ya simu ni milioni 30.5 ambapo thamani ya miamala katika kipindi hicho ilikuwa Shilingi trilioni 11.5 yenye wastani wa Shilingi 377,795 kwa kila muamala.
"Inatarajiwa uwepo wa mfumo wa kuuza na kununua hisa kwa njia ya simu za mkononi kutawavutia wananchi wanaofanya miamala hii kuwekeza sehemu ya fedha hizi kwenye soko la hisa, na hivyo kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Sekta ya Masoko ya Mitaji katika Mpango wa Kitaifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha 2018 – 2022 unaolenga kuongeza kwa asilmia 50, wawekezaji katika masoko ya mitaji.
"Kwa kuwa mfumo huu unatarajia kuwezesha kuongezeka kwa miamala katika Soko la hisa, inatarajiwa kwamba ukwasi wa Soko la hisa utaongezeka. Ukwasi mkubwa wa Soko ni kiashiria muhimu cha ubora wa soko kinachovutia wawekezaji wengi wa ndani na wa kimataifa,"amesema
Ameongeza Mfumo huo wa Hisa Kiganjani unatarajiwa kuongeza mchango katika jitihada za kuongeza uelewa na elimu ya fedha kwa umma, zinazofanywa na DSE na CMSA. Baadhi ya jitihada hizo ni pamoja na mipango ya Shindano la Masoko ya Mitaji Kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu .Shindano la Uwekezaji kwa Wanafunzi linaloendeshwa na Soko la Hisa la Dar es Salaam; na Mpango wa DSE wa Kuendeleza Biashara yaani the DSE Enterprise Acceleration Program.Matumizi ya Mfumo huu yatawezesha kufikiwa kwa haraka zaidi kwa malengo ya mipango hii.
Ametoa rai kwa soko la Hisa na Wadau wote katika Masoko ya Mitaji kuhakikisha kuwa mfumo huu unaleta tija na manufaa yafuatayo yakiwemo ya kupunguza gharama za shughuli za uwekezaji, kuondoa changamoto ya ulazima wa wawekezaji kuwa karibu na Soko au watoa huduma za kununua na kuuza hisa.
Pia kuongeza hamasa ya uwekezaji kwa kundi la vijana ambao ndio wengi katika jamii, kuwezesha Watanzania waliopo nje ya nchi kushiriki katika uwekezaji hapa nyumbani na kujenga utamaduni wa wananchi kuwekeza kutokana na urahisi wa namna ya kuwekeza katika soko la hisa.
"Ili kufikia malengo hayo, natoa mwito kwa Uongozi wa Soko la Hisa la Dar es Salaam na kampuni zote zenye leseni kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana kuhamasisha matumizi ya Mfumo huu ikiwa ni pamoja na kuingiza elimu ya matumizi yake kwenye mipango yao ya kila mwaka ya elimu kwa umma.
"Napenda kutumia fursa hii kuwataka watanzania wote, waliopo ndani na nje ya nchi, kutumia mfumo huu mpya kwani sasa huduma imeletwa mikononi mwetu kupitia HISA KIGANJANI. Kama sote tunavyoolewa matumizi ya huduma za kifedha ni moja ya nyenzo kuu ya kupata maendeleo ya mtu mmoja na Taifa kwa ujumla.
"Muitikio wa Watanzania utaleta hamasa kwa Serikali na Wadau wake ikiwa ni Pamoja na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana katika kuongeza juhudi zaidi katika kutafuta mbinu bora zaidi za huduma na bidhaa za masoko ya hisa kwa Wananchi,"amesema.
Ametoa msisitizo kwa Soko la Hisa, Taasisi zinazotoa huduma katika soko la hisa, na Wadau wa Sekta ya Masoko ya Mitaji kuwa Dunia hivi sasa ipo kwenye Mapinduzi ya Nne ya Viwanda.
"Shughuli nyingi ulimwenguni na kimataifa, kwa sasa, zinafanyika kwa kutumia TEHAMA. Hivyo basi, wadau wote wa sekta ya masoko ya mitaji wanapaswa kwenda na kasi hiyo ya kukua kwa sekta ya mawasiliano ya Tehama. Kwa mantiki hiyo wadau wote mnapaswa kubuni bidhaa na huduma zinazoendana na kasi ya kukua kwa sekta ya mawasiliano ya Tehama ulimwenguni.
"Serikali kupitia Mamalaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA) itaendelea kujenga mazingira wezeshi na shirikishi kwa lengo la kufikia azma hiyo kwa maendeleo ya masoko ya mitaji hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wetu hapa nchini,"amesema.
0 comments:
Post a Comment