Ikulu
imevunja ukimya kuhusu ile sinema ya kuahirishwa mfululizo kwa uchaguzi
wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam kwa kusema haitaona tatizo lolote
iwapo Halmashauri hiyo itaongozwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa).
Uchaguzi
huo utakapofanyika na vyama hivyo kushinda na kuongoza Jiji, Ikulu
imesema, hakutaathiri hata kidogo shughuli zake za kila siku hivyo haina
mkono wake kwenye sarakasi za uchaguzi huo.
Hayo
yalisemwa jana na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue,
alipoulizwa ni kwanini Ikulu isiingilie kati na kuamuru kufanyika kwa
uchaguzi huo ambao umeshapigwa danadana muda mrefu.
“Hilo la hisia kwamba Ikulu ina mkono wake kwa kuhofia Ikulu kuwa chini ya Ukawa si kweli hata kidogo,” alisema Balozi Sefue.
"Sisi tuogope nini wakati wao hawataathiri shughuli zetu za kila siku? Nakuhakikishia hatuoni tatizo lolote."
Kumekuwa
na tetesi kwamba serikali inahofia upinzani kuchukua Jiji, kwani Ikulu
ni kama itakuwa ndani ya eneo linalotawaliwa na wapinzani hali
itakayoleta mgongano wa kiutendaji na kimaslahi.
Balozi
Sefue alisema Jiji kuongozwa na Ukawa hakuwezi kuwanyima usingizi hata
kidogo kwasababu iko miji mingi mikuu duniani ambayo inaongozwa na vyama
vya upinzani na shughuli za Ikulu kwenye miji hiyo zinaendelea kama
kawaida.
“Sisi
hatuhofii na wala hatuoni sababu ya kuingilia uchaguzi huo ati kwa
kuhofia Ukawa kuongoza Jiji, mbona miji mbalimbali duniani inaongozwa na
vyama vya upinzani na mambo yanakwenda kama kawaida?" Alihoji.
"Sisi hatutakuwa wa kwanza duniani na wala hakuna kitakachobadilika.”
Kuhusu
zoezi hilo kutawaliwa na ubabaishaji, Balozi Sefue alisema kwa sasa
Ikulu haiwezi kuingilia kati na kulazimisha siku ya uchaguzi huo
kwasababu wahusika wapo na hawajasema kama wameshindwa.
“Waziri anayehusika na Tamisemi yupo na hasema kwamba ameshindwa. Sasa kwanini sisi tuingilie suala lao?
"Mimi naamini hawajashindwa na wakishindwa wenyewe wanajua waende wapi kwa ajili ya ufumbuzi.
Mvutano
wa Umeya wa Jiji umetokana na vyama vinavyounda Ukawa kuvuna madiwani
wengi kuliko CCM katika jiji la Dar es Salaam hivyo kuwa na uwezekano
mkubwa wa kutwaa Halmashauri ya Jiji, ikiwa uchaguzi huo utafanyika kwa
uhuru na haki.
Jiji lina madiwani 76 wa CCM wakati Ukawa ina 87.
Tayari
Halmashauri mbili kati ya tatu za Dar es Salaam zinaongozwa na Ukawa:
Ilala na Kinondoni wakati CCM ikiongoza Temeke pekee.
Hata
idadi ya wabunge kwa Dar es Salaam, Ukawa imeizidi kwa mbali CCM ambayo
imepata wabunge wanne tu ambao ni Faustine Ndungulile wa Kigamboni,
Issa Mangungu (Mbagala), Bona Kaluwa (Segerea) na Mussa Azan Zungu
(Ilala).
Katika
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana Ukawa ilichukua majimbo ya Kawe
linaongozwa na Halima Mdee (Chadema), Ukonga la Mwita Waitara (Chadema),
Ubungo la Saed Kubenea (Chadema), Kibamba la John Mnyika (Chadema) na
Kinondoni la Maulid Mtulia (CUF).
Katika
kuonyesha kuwa sakata hilo bado ni moto, madiwani na wabunge wanaotoka
Ukawa, juzi walivamia ofisi za Jiji wakishinikiza waambiwe tarehe ya
uchaguzi huo.
Wanachama
hao wa Ukawa walikaa kwa saa nzima kwenye ofisi hizo bila kupata jibu
kutoka kwa wahusika na walisikika wakilaumu uongozi wa Jiji kuwa
umepanga kuwahujumu.
Ingawa
Ikulu ilisema kuwa haiwezi kuingilia suala hilo kwa kuwa Waziri husika
hajashindwa, kuna dalili kwamba waziri mwenye dhamana amenawa mikono na
hajui namna ya kutatua tatizo hio
Jiji
liko chini ya Tamisemi ambayo iko Ofisi ya Rais hivyo kumekuwa na hofu
kwamba iwapo Ukawa watachukua kiti cha Meya, kutakuwa na mgongano mkubwa
wa sera na utekekelezaji wa ilani ya upinzani na ya Ukawa.
Vyama
vya Ukawa vilishatoa angalizo hivi karibuni kwamba serikali inajaribu
kutengeneza mgogoro ili kumpa nafasi Rais John Magufuli kuvunja
Halmashauri ya Jiji na kuunda tume ya jiji.
Sheria ya Tamisemi ya mwaka 1982 inampa mamlaka Rais kuvunja Halmashauri ya Jiji/Mji/Manispaa na kisha kuteua tume.
Mwaka
1996, Fredrick Sumaye, akiwa Waziri Mkuu, aliivunja Halmashauri ya Jiji
la Dar es Salaam na kuunda tume iliyoongozwa na Charles Keenja.
Wiki
iliyopita ziliibuka vurugu za kurushiana makonde kati ya wafuasi wa
Ukawa na Polisi kufuatia kuahirishwa kwa uchaguzi huo kutokana na madai
ya kuwepo zuio la muda Mahakama lilowekwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM),
ambalo baadaye ilibainika kwamba lilikuwa feki.
Kabla
ya wiki iliyopita, uchaguzi wa Meya wa Jiji ulishaahirishwa mara moja
kwa sababu za kiujanja ujanja kutokana na pingamizi la CCM.
0 comments:
Post a Comment