Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli
Tanzania (Rahco), Benhadard Tito na wenzake wawili wamepadishwa
kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na
mashtaka manne.
Vigogo wawili wa Rahco na mfanyabiashara
wanakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka,
kula njama na kusababisha hasara ya dola za Marekani 527,540.
Mbali
na Tito, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwanasheria wa Rahco,
Emmanuel Massawe na mfanyabiashara ambaye pia ni mwakilishi wa kampuni
ya Rothschild (South Africa) Proprietary Limited, Kanji Mwinyijuma.
Washtakiwa
hao watatu walisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas
Simba, huku upande wa mashtaka ukiwa na Maghela Ndimbo, Janeth Machulya
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kushirikiana
na Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis.
Mawakili hao,
wakiongozwa na Vitalis walidai kuwa washtakiwa wote watatu katika
nyakati tofauti kati ya Septemba Mosi, 2014 na Septemba 30, 2015 katika
Mkoa wa Dar es Salaam walikula njama ya kutenda makosa hayo chini ya
Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Katika kesi hiyo,
ilidaiwa kuwa Februari 27, 2015, Tito katika ofisi za Rahco zilizoko
wilayani Ilala, alitumia madaraka yake vibaya kwa kuipitisha kampuni
hiyo ya Rothschild kama mshauri wa mradi wa uimarishaji wa Reli ya Kati
bila idhini ya Bodi ya zabuni ya Rahco, hivyo kwenda kinyume na Sheria
ya Manunuzi ya Umma.
Tito na Massawe wanadaiwa kuwa Machi 12,
2014 katika ofisi hizo za Rahco walitumia madaraka yao vibaya kwa kutia
saini barua rasmi ya kuichagua kampuni hiyo, kama mshauri katika
mchakato wa uimarishaji wa njia ya Reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa
(standard gauge).
Kati ya Machi 12 na Mei 20, 2015 katika ofisi
za Rahco, Tito na Massawe wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa
kushindwa kuwasilisha mkataba wa huduma ya ushauri, baina ya kampuni
hizo mbili kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Pia wanadaiwa
kuwa kati ya Mei 20 na Juni 20, 2015 katika ofisi hizo washtakiwa hao,
walishindwa kuwasilisha nakala ya mkataba kati ya kampuni hizo kwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mbali na
mashtaka hayo, washtakiwa hao kwa pamoja kwa nyakati tofauti kati ya
Machi Mosi na Septemba 30, 2015 walitoa huduma ya ushauri kwa kampuni
hiyo, bila kufuata taratibu za ununuzi na malipo na walisababisha hasara
ya dola za Marekani 527,540 ambazo zililipwa kama gharama za malipo ya
awali.
Agosti 18, 2015, Tito akitekeleza majukumu yake, alitumia
vibaya mamlaka kwa kuipatia kampuni ya China Railway Construction
Corporation kazi ya ujenzi wa reli kwa kilomita mbili za kiwango cha
kisasa kutoka Soga, iliyogharimu dola Marekani 2, 312,229.39 bila ya
kuwa na idhini ya bodi ya zabuni ya Rahco.
Washtakiwa
hao hawakuruhusiwa kujibu kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya
kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu. Uamuzi wa dhamana utatolewa
Ijumaa.
0 comments:
Post a Comment