WAKATI Rais John Magufuli, Baraza la Mawaziri na viongozi wengine wakiombewa ili kufanya kazi vizuri katika ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika jana, viongozi mbalimbali wamekumbushwa kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia wananchi kwa haki bila kushinikizwa.
Akihubiri katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Maxmillian Maria Kolbe, Mwenge jijini Dar es Salaam, Askofu Msaidizi, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa, alisema ni vyema viongozi katika jamii wakumbuke wamepewa dhamana ya kuangalia wengine na kuongoza kwa haki na kuacha tabia ya ubinafsi na maamuzi ya kushinikizwa.
“Sisi tuliopewa dhamana tuamue kwa haki na kamwe tusiamue kwa shinikizo, kwa sababu ni heri kufa shahidi kuliko kuangamiza damu za watu wasio na hatia,” alisema Askofu Nzigilwa katika Ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika kitaifa kanisani hapo.
Aliwataka waumini kutumia Ibada ya Ijumaa Kuu kuwa kiele- lezo cha upendo kwa wengine na kamwe usaliti usiwepo kwa kuwa ni jambo baya lin- aloleta uharibifu. Alisema usaliti uliofanywa na Yuda Iskariote wa kumbusu Yesu Kristo, ni jambo gumu linalotakiwa kuepukwa na wanadamu kwa sababu ni sumu inayoua.
“Matendo ya unafiki na usaliti ni mabaya, kwa sababu mtu au watu wanaofanya huyafanya dhidi ya wengine huku mkichekeana, lakini kwa ndani unamuua, tafadhali tusiwe na sura mbili, kama ni ndiyo iwe ndiyo na sio iwe sio,” alisema Askofu Nzigilwa.
Naye Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa, amewataka Watanzania hasa waumini wa dini ya Kikristo kuachana na dhambi na kuishi katika uadilifu unaompendeza Mungu.
Akizungumza baada ya misa ya Ijumaa Kuu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Albano, Askofu Mokiwa alisema, kuna kila haja ya watu kubadilika na kuachana na maisha ya dhambi kwa kuwa hayampendezi Mungu.
Naye Padre Nicholaus Masamba wa katika Kanisa Kuu Katoliki la Mtakatifu Joseph, aliwataka Watanzania kutekeleza wajibu wao katika mambo mbalimbali ili kuhakikisha familia zinakua na maadili mazuri.
“Wazazi wanatakiwa kuhakikisha watoto wanalelewa katika malezi bora ili kuendana na tafakari ya Yesu iliyosema yametia wakati anakata roho baada ya kutimiza wajibu wake,” alisema.
Katika Kanisa la Kiinjili la Kiletheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Azania Front, Mchungaji wa kanisa hilo, Charles Mzinga, aliwataka Wakristo kumtegemea Mungu katika kila jambo wanalopitia na kulifanya kwa kuwa ndio nguzo muhimu katika maisha ya binadamu.
Alisema ibada hiyo inawakumbusha mateso na kifo cha Yesu hivyo kila mmoja anapaswa kumpokea na kumtegea katika maisha yake.
Magufuli aombewa
Katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kipawa Kigango cha Stakishari, Mlezi na Mhadhiri wa Seminari Kuu ya Mtakatifu Karoli Lwanga, Segerea, Padre Peter Msafiri, aliwataka Wakristo kuombea Serikali inayoongozwa na Rais Magufuli.
Aliwataka pia kuwaombea mawaziri, makatibu wakuu na wakuu wote wa vitengo serikalini, ili Mungu awaongeze kwenye utendaji kazi wao.
Wakati katika Kigango cha Stakishari wakifanya sala maalumu ya kumuombea Rais Magufuli na Serikali yake, Rais Magufuli pamoja na mke wake, Janeth Magufuli, walishiriki ibada ya Ijumaa Kuu katika Kanisa la Mtakatifu Petro, jijini Dar es Salaam.
Katika ibada hiyo, mbali na Rais Magufuli na mke wake, viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na mke wa Waziri Mkuu, mawaziri na wabunge.
Mkoani Morogoro, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Telesphor Mkude juzi katika ibada ya Alhamisi Kuu, aliwaasa waumini kuonesha dhamira ya kujishusha na kuhudumia wadogo.
Mkude alisema Yesu Kristu anataka unyenyekevu huo katika jumuiya, katika familia na jamii nzima kwa ujumla ambapo alisema kuwa wanapaswa kutoa sadaka ya kuhudumiana.
Uchaguzi Zanzibar
Nako huko Dodoma Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Dodoma, Mchungaji Samwel Mshana ameshauri vyama ambavyo havikushiriki uchaguzi wa Zanzibar kuingizwa katika serikali ya Umoja wa Kitaifa, kwani nao wana nafasi kubwa ya kujenga uchumi amani na ustawi wa Zanzibar.
Katika mahubiri yake pia aliwakumbusha waumini kuiona Pasaka hiyo kama sehemu ya kujihoji kwenye matendo wanayoyafanya kama kuna mahusiano yoyote na Mungu badala ya kuichukulia kuwa ni sikukuu kama zingine.
Naye Askofu mstaafu wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tabora, Francis Ntiruka alishauri serikali ya Unguja kuachana na siasa na badala yake iwatumikie wananchi. Askofu huyo aidha amemtaka Rais wa Zanzibar kujali na kuwatimizia mahitaji wananchi wote kama alivyoahidi bila kujali kama kuna vyama ambavyo vilisusia uchaguzi huo.
Aidha amewataka Wakristo kuhakikisha wanaitumia Pasaka kwa kutenda mema na kuonesha upendo kwa vitendo huku wakijiepusha matendo yasiyofaa kama vile ulevi uasherati wizi ikiwemo na matumizi ya madawa ya kulevya.
Imeandikwa na Ikunda Erick, Regina Kumba, Theopista Nsanzugwanko na Katuma Masamba Dar, Agnes Haule, Morogoro na Sifa Lubasi, Dodoma.
0 comments:
Post a Comment