Mahakama Kuu inatarajia kusuluhisha kesi iliyofunguliwa na Kampuni ya
Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) dhidi ya Mbunge
wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe na wenzake Machi 23, mwaka huu.
Kesi
hiyo namba 175 ya mwaka 2014 ilipangiwa kuanza kufanyiwa usuluhishi
jana mbele ya Jaji Salvatory Bongole, lakini ilishindikana kutokana na
upande wa walalamikaji ambao ni IPTL kushindwa kufika mahakamani.
Hata
hivyo, Kaimu Msajili wa Mahakama hiyo Kitengo cha Usuluhishi, Beda
Nyaki alisema kesi hiyo itasikilizwa kwa siri baina ya pande hizo.
“Kesi
hii haiwezi kuripotiwa kwenye vyombo vya habari kwa sababu ipo katika
hatua za kwanza za usuluhishi, hivyo kitu kitakachoongolewa baina ya
walalamikaji na walalamikiwa kitakuwa ni siri yao,” alieleza Nyaki.
Alisema kusikilizwa kwa faragha kwa kesi hiyo ni hatua ya kupunguza gharama na muda.
Katika
kesi hiyo, Kampuni za IPTL, Pan Africa Power Solutions (T) Limited na
Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hizo, Harbinder Sing Seth walifungua
madai ya Sh500 bilioni dhidi ya Zitto, Mhariri wa gazeti la Raia Mwema,
Kampuni ya Raia Mwema na Kampuni ya Flint Graphics ikiwa fidia kwa
kuwakashfu kuhusiana na sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh300 bilioni
katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Mawakili wanaomtetea Zitto ni
Wakili Ntemi Masanja na Ivone Sianga ambao walidai kuwa walalamikaji
walishindwa kufika mahakamani hapo na kusababisha kuahirishwa kwa kesi.
Ilidaiwa
kuwa walalamikaji hao walichukua hatua ya kufungua kesi hiyo kufuatia
makala aliyoyaandika Zitto katika gazeti la Raia Mwema la Agosti 13,
2014 katika ukurasa wa saba na wa 14, ikiwa na kichwa cha habari “Fedha
za IPTL ni mali ya umma.’’
Walalamikaji hao walidai kuwa makala hiyo ni ya upotoshaji na ilikuwa na lengo la kuwachafua mbele ya jamii.
0 comments:
Post a Comment