Wanafunzi nane wa Shule ya Sekondari Kiwanja, wilayani Chunya, wamefukuzwa shule kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo kuchoma mabweni ya shule hiyo pamoja na kukutwa na simu na vitu vingine ambavyo haviruhusiwi shuleni.
Uamuzi huo umetangazwa jana shuleni hapo na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, alipoenda kuangalia maendeo ya ukarabati wa mabweni hayo ambapo amesema uamuzi huo umefanywa na Bodi ya Shule hiyo kabla haijavunjwa.
Chalamila amesema wanafunzi saba kati ya waliofukuzwa wanakabiliwa na kesi ya kuchoma mabweni ya shule mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu na kuisababisha serikali hasara kubwa. Na mwanafunzi mmoja amefukuzwa kosa la kukutwa na simu pamoja na kondomu kwenye begi lake wakati akirejea shuleni.
“Hao wote wanaokabiliwa na kesi wamefukuzwa, lakini wanaunganishwa na huyo ambaye alirejea tena shuleni akiwa na simu kwenye begi lake pamoja na kondomu, inaonyesha hii shule mnabakana sana, sasa ole wenu tuje tuwakamate” amesema Chalamila.
Aidha, Chalamila amesema kwa wanafunzi ambao bado hawajakamilisha malipo yao hawataruhusiwa kuingia darasani mpaka Novemba 1, mwaka huu ambapo watatakiwa kupeleka risiti za malipo na barua ya kukiri kosa na kueleza sababu ya kwanini wamechelewa. Na endapo watakiuka agizo hilo Bodi ya Shule itatakiwa ikae na kufanya maamuzi mengine dhidi yao ikiwa ni pamoja na kufukuzwa shule.
Hata hivyo, amewapa wiki moja wanafunzi ambao bado hawajakamilisha malipo ya fedha za kukarabati mabweni yaliyoteketea kwa moto kuhakikisha wanakamilisha ili waendelee na masomo.
Mkuu wa Shule hiyo, Elly Mnyarape amewataja wanafunzi waliofukuzwa shule kuwa ni Loren Msechu, Barnaba Minga, Samwel Ibrahim na Osward Msomba kidato cha sita, James Kunambi na Baraka Kasisike kidato cha nne.
Na kijana aliyekutwa na simu pamoja na kondomu kwenye begi lake baada ya kurejea kuwa ni Peter Kabimilo wa kidato cha sita ambaye amekimbia na hajulikani alipo.
0 comments:
Post a Comment