Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) jana tarehe 22 Februari 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani Afrika-AGRA Kanda ya Mashariki na kati inayojumuisha mikoa ya Tanzania, Rwanda na Uganda Prof Nuhu Hatibu sambamba na Mkuu wa Shirika la Chakula Duniani nchini Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa wafadhili wa maendeleo upande wa kilimo- Tanzania Ndg Fred Kafeero.
Katika Mkutano huo Waziri Hasunga ameeleza dhamira ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli imeanza zoezi la kuwatambua na kuwasajili wakulima wa mazao yote nchini lengo likiwa ni kuwatambua ili kupanga mipango sahihi yenye kuongeza tija na uzalishaji katika mazao yote.
Hasunga alitoa agizo hilo tarehe 29 Disemba 2018 wakati akizungumza na Wenyeviti wa Bodi za Mazao pamoja na Wakurugenzi wa Bodi hizo za Mazao, kwenye ukumbi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Jijini Dodoma.
Mhe. Hasunga alisema ili kuongeza tija na uzalishaji katika Sekta ya kilimo na kuandaa mipango madhubuti ya kuendeleza mazao yote ni vyema kuwatambua Wakulima wote nchini na kuongeza kuwa Wakulima wa zao la korosho wametoa funzo kubwa kwa Wizara yake kufanya jambo kama hili katika mazao mengine hapa nchini.
Waziri Hasunga aliongeza kuwa mipango sahihi ya kuwaendeleza Wakulima kuanzia kwenye kilimo chenyewe hadi kufikia katika hatua ya kuvuna, kuhifadhi na kulifikia soko ni vyema kuwa na mfumo maalumu wa kanzi data (Database) ya kuwafahamu ili kushughulikia mahitaji yao kisasa na kwa haraka zaidi.
Vilevile ameeleza umuhimu wa kuanzishwa kwa Sheria ya Kilimo itakayotoa suluhisho la changamoto zinazamkabili Mkulima na Sekta hiyo kwa ujumla. “Kuna kila sababu ya kuanzishwa haraka sheria ya kilimo, kwa sababu hatuna Sheria ya Kilimo na inayotumika sasa ni Sera ya Kilimo, iliyotungwa mwaka 2013 ambayo pia inahitaji kupitiwa upya” Alisema
Alisitiza pia kuwa serikali imedhamiria kuanzisha Bima ya mazao ya wakulima nchini kwani hiyo ni hatua nzuri katika kuhuisha utoaji wa huduma bora za bima za kilimo kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Bima ya Mwaka 2009, Sheria na Mipango Mbalimbali katika sekta ya kilimo; kwa kutafutia ufumbuzi wa pamoja changamoto zinazokabili sekta ya kilimo na wakulima nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani Afrika-AGRA Kanda ya Mashariki na kati inayojumuisha mikoa ya Tanzania, Rwanda na Uganda Prof Nuhu Hatibu amempongeza waziri wa kilimo huku akisisitiza kuwa AGRA inaunga mkono zoezi la usajili wa wakulima na ipo tayari kushirikiana na serikali katika zoezi hilo.
Naye, Mkuu wa Shirika la Chakula Duniani nchini Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa wafadhili wa maendeleo upande wa kilimo- Tanzania Ndg Fred Kafeero amesema kuwa shirika hilo litaendeleza ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika kuiinua sekta ya kilimo nchini.
Katika hatua nyingine Mhe Hasunga amekutana na kufanya mazungumzo na aliyewahi kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt Fenela Mkandalla.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment