Wednesday 27 February 2019

MWANAFUNZI AUAWA KWA KUPIGWA NA KIRANJA SHULENI

...
 Hali ya majonzi imeikumba Shule ya Sekondari St Joseph Nyabigena iliyopo Gucha Kusini, Kaunti ya Kisii nchini Kenya kufuatia kifo cha mwanafunzi mwenzao anayedaiwa kupigwa na kiranja.

 Mwanafunzi huyo wa kidato cha tatu anadaiwa kuaga dunia baada ya kukimbizwa katika Hospitali ya Wamisionari ya Tabaka.

Kwa mujibu wa ripoti ya Nation, marehemu alianguka na kuzimia baada ya kupigwa na kiranja, na inadaiwa walizozana kabla ya kisa hicho asubuhi ya Jumanne 26,2019.

 “Marehemu alikuwa akisoma Bibilia kuelekea saa moja asubuhi. Baada ya mgogoro kidogo kati yao kiranja alimpiga kofi kisha teke la tumbo na hapo alianguka na kuzimia,” mmoja wa wanafunzi alisema.

 Usimamizi wa hospitali ulikataa kusema na wanahabari kuhusu kilichosababisha kifo cha mwanafunzi huyo.

 Kamanda wa Polisi wa Kaunti Martin Kibet alithibitisha kutokea kisa hicho na kusema tayari uchunguzi wa polisi umeanzishwa. 

“Tunafahamu kuhusu kisa hicho na tumewaruhusu polisi kufanya uchunguzi wao kabla ya kutoa taarifa.” Kibet alisema.

 Mwalimu Mkuu Mathew Simiyu alitoweka katika shule hiyo mara baada ya tukio hilo na wanahabari hawakupata fursa ya kusema naye.

 Mwalimu ambaye hakutaka jina lake kutajwa alisema, mwalimu mkuu alizungumza na wanafunzi na kuwataka kuwa watulivu kabla ya kuondoka.

 Baadhi ya walimu waliozungumza na wanahabari waliwalaumu walimu wakuu kwa kuwapa mamlaka mengi viranja.

 “Waliohusika wakamatwe na kusema kilichotokea. Ni makosa kwa wanafunzi kupewa idhini ya kuwaadhibu wanafunzi wengine,” mmoja wa walimu alisema.

 Wanafunzi walisusia chakula cha mchana na kulalamika kuhusu viranja kuwafanyia ukatili shuleni. 

Maafisa wa Polisi kutoka Kituo cha Polisi cha Nyamarambe walimhoji mwalimu aliyekuwa zamu kuhusu tukio hilo lakini haikubainika iwapo yeyote ametiwa nguvuni kuhusiana na kifo cha mwanafunzi huyo.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger