Tuesday 26 February 2019

MTOTO ALIWA NA MAMBA AKIOGA ZIWANI

...
Mwanafunzi wa darasa la pili Shule ya Msingi Nyambeba katika halmashauri ya Buchosa mkoani Mwanza, Stivine Wiliam (10) amekufa kwa kuliwa na mamba alipokuwa akioga ndani ya Ziwa Victoria.

Kufariki kwa mtoto huyo kumefikisha idadi ya watu waliopoteza maisha kwa kuliwa na mamba kufikia 14 tangu mwaka 2016 hadi sasa.

Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole aliiambia Mwananchi jana Jumatatu, Februari 25 kuwa Serikali inaangalia uwezekano wa kutunga sheria ndogo kukataza watu kuoga ndani ya Ziwa Victoria kama moja ya hatua za kukabiliana na matukio hayo.

Akizungumzia tukio la mtoto huyo kukamatwa na kuliwa na mamba, Afisa Mtendaji Kijiji cha Nyambeba, Edward Pastory alisema tukio hilo lilitokea saa 10:00 jioni ya Februari 22, 2019.

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, jumla ya watu watano wamepoteza maisha wilayani Sengerema kwa kuliwa na mamba.

Kaimu Afisa Ardhi na Maliasili Halmasahuri ya Buchosa, Ariko Ndile alitaja maeneo yanayokumbwa na matukio hayo kuwa ni vijiji vya Nyambeba, Kanyala, kisaba, Izindabo na Kisiwa cha Kome katika kata ya Buhama.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Buchosa, Crispin Luanda alisema ofisi yake imeanza kuchukua hatua kwa kuchimba visima 14 katika maeneo mbalimbali kuwezesha wananchi kupata huduma ya maji badala ya kutegemea huduma hiyo ziwani.
Na  Daniel Makaka, Mwananchi 
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger