Bibi kizee alivyonaswa usiku akirandaranda na tunguri nyumbani kwa Waziri Mwigulu Nchemba.
Stori: Francis Godwin, Risasi Jumamosi
DODOMA: Katika hali
isiyo ya kawaida bibi kikongwe mmoja ambaye hakuweza kujulikana jina
lake, amezua sintofahamu baada ya kukutwa nyumbani kwa Waziri wa Kilimo,
Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba akizunguka nyumba yake usiku huku
akiwa na tunguri na wembe wenye damu.
Tukio
hilo lilitokea Mei 31, mwaka huu majira ya saa 6 usiku katika eneo la
Kilimani mjini Dodoma kwenye nyumba ya waziri huyo ambako ni makazi ya
mawaziri na viongozi mbalimbali wa umma.
Akizungumza na mwandishi wetu, eneo la
tukio, shuhuda wa tukio hilo, Sumai Juma alisema kuwa alimwona mwanamke
huyo akiwa amekumbatia vitu vyake akizunguka nyumba ya waziri.
Baada
ya kumwona mtu huyo, alilazimika kuita mlinzi na kujaribu kumhoji bila
mafanikio kutokana na mwanamke huyo kutojua lugha yoyote na kila
anachoulizwa alikuwa hajibu zaidi ya kurudia maneno yaleyale ambayo
alikuwa akimuulizwa.
“Huyu
kikongwe alikuwa kama na zaidi ya miaka 70 hivi, nilimwona akiwa
amesimama katika dirisha la mheshimiwa waziri na baada ya kumfuata
alianza kuzunguka nyumba hiyo asijue mlango wa kutokea…nyumbani hapa
kuna uzio mrefu sana ambao bibi kama huyu hana uwezo wa kupanda na
getini muda wote kuna walinzi wa Kampuni ya Moku Security ambao
hawakumwona akiingia getini hapo,” alisema Juma.
Hata hivyo, alisema baada ya kumkamata
walichunguza mzigo aliokuwa amebeba ambao ulifungwa katika kanga,
kulikuwa na kuni kama 17 hivi, kikopo chenye vitu kama ungaunga mweusi
mfano wa vumbi, mkaa na wembe aina ya Topaz uliokuwa haujafunguliwa ila
ulikuwa umelowa damu.
Juma
aliongeza kuwa, baada ya kumkagua na kutokana na mtu huyo kutojitambua,
walilazimika kumpeleka Kituo cha Polisi Dodoma ambako walimweka
mahabusu baada ya kushindwa kujieleza na asubuhi Waziri Nchemba
alilazimika kwenda kuruhusu kuachiwa huru baada ya kumsamehe.
Kwa
upande wake Waziri Nchemba alisema ameshindwa kujua lengo la mwanamke
huyo katika nyumba yake lakini yeye hana hofu yoyote kwani yupo kwa
ajili kuwatumikia wananchi kwa nafasi yake ya uwaziri na hivyo kazi yake
anayoifanya anaiweza kwa kuwa anamtanguliza Mungu mbele.
Hata hivyo, alitoa wito kwa Watanzania
kuendelea kuliombea taifa kwani kazi kubwa ambayo serikali ya Rais Dk.
John Pombe Magufuli inayofanya ni tunu kubwa ya nchi yetu.
0 comments:
Post a Comment