Tuesday 28 June 2016

MECHI YA YANGA VS TP MAZEMBE: Mashabiki Kuingia Uwanjani Bure Leo, Kikomo cha Mashabiki ni 40,000 Ukichelewa "Tazama Kwenye TV"

...

MASHABIKI wa Yanga leo watajazana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam bila kulipa hata senti tano kushuhudia mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Hata hivyo, kujazana kwao uwanjani hakutakuwa na maana iwapo kikosi hicho cha Kocha Hans van der Pluijm kitashindwa kuondoka na pointi tatu.
Katika mchezo wa kwanza wa mashindano hayo dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria, Yanga ililala kwa bao 1-0, hivyo mechi ya leo kuwa na kila sababu ya kushinda hasa kwa kuzingatia itakuwa mbele ya mashabiki wake wengi.
Awali, kulikuwa na mvutano kati ya Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya klabu hiyo ya Jangwani kutangaza kuwa mashabiki wataingia bure.
Hata hivyo, makubaliano ya mwisho yaliyolishirikisha pia Shirikisho la Soka Afrika (Caf), mashabiki wasiozidi 40,000 ndiyo watakaoruhusiwa kuingia uwanjani kutokana na sababu za kiusalama, kwa mujibu Msemaji wa TFF, Alfred Lucas.
Lucas alisema kamisaa wa mchezo huo kutoka Zambia, Kidio Joseph alikuwa na shaka huenda uwanjani ungejaa kupia uwezo, hivyo kuhatarisha usalama.
"Hayo ni maelekezo tuliyoyapata kutoka CAF na Yanga wanazo taarifa hizi na ni lazima tufuate maelekezo hayo," alisema Lucas.
Aidha, alisema mashabiki wataruhusiwa kukaa kwenye jukwaa la mzunguko na majukwaa mengine watakaa watu maalum (Special Seat).
Aidha, kwa upande wa Yanga wamekubali maelekezo hayo ya CAF.
Afisa habari wa timu, Jerry Muro, alisema wamepata taarifa hiyo ya CAF na hawana pingamizi nayo.
Achana na habari hiyo, turudi kwenye mchezo wa Yanga na Mazembe.
Wawakilishi hao wa Tanzania, wataingia uwanjani wakiwa na dhamira moja tu ya ushindi, kwani hata matokeo ya sare dhidi ya timu hiyo ngumu hatawasaidia kujiweka kwenye nafasi nzuri.
Pluijm alisema wachezaji wake wanafahamu umuhimu wa ushindi kwenye mchezo huo, kinyume na ushindi basi vijana hao wa Jangwani watakuwa wamepotea njia.
"Kupoteza mchezo wa kesho (leo) itakuwa mbaya zaidi kwetu, kundi letu lina timu nne na kati ya hizo mbili zilipata ushindi kwenye mechi zao za kwanza," alisema Pluijm.
Pluijm, ambaye kikosi chake kiliweka kambi zaidi ya wiki mbili nchini Uturuki kujiandaa na michuano hiyo, ana matumaini wakubwa wachezaji wake watafuata maelekezo yake na kushinda mechi hiyo.
"Wachezaji wangu wako kwenye hali nzuri, wamejiandaa kikamilifu kwa mchezo huu. Ukimuondoka Msuva (Simon), wengine wako kwenye hali nzuri kimchezo," alisema na kuongeza:
"Tunahitaji kushinda leo mbele ya mashabiki wetu waliopata fursa ya kuingia uwanjani bila kulipa kiingilio. Haitakuwa na maana kupoteza mchezo huu, siyo tu kwa sababu mashabiki wetu wataingia uwanjani bura, bali matokeo ya kipigo yatatuweka kwenye wakati mgumu."
TP Mazembe wanashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu ya ushindi baada ya kushinda mchezo wa kwanza, hivyo wamejipanga kikamilifu kuifunga Yanga nyumbani
Katikati ya wiki hii, mshambuliaji Mazembe, Thomas Ulimwengu alisema mchezo utakuwa mgumu kutokana na ukweli kwamba Yanga ni timu nzuri na hawatakubali kupoteza mchezo mwingine baada ya kushindwa kupata pointi kwenye mchezo wa kwanza.
"Tumejiandaa vizuri na mchezo huu, pamoja ya kuwa mpira una matokeo matatu lakini kwetu tunaamini kwenye ushindi," alisema Ulimwengu.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger