Tuesday 21 June 2016

CHADEMA Wataka Mkutano Mkuu wa CCM Kumkabidhi Uenyekiti Magufuli Nao Uzuiliwe

...


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetoa tamko zito kikitaka Polisi kuzuia Mkutano Mkuu wa CCM utakaofanyika mwezi ujao, vinginevyo watatumia nguvu ya umma kuuzuia.

CCM kimeitisha mkutano mkuu maalumu unaotarajiwa kufanyika Julai 23 mjini Dodoma, kwa lengo la Mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Kikwete kumkabidhi uongozi wa chama, Rais John Magufuli.

Kauli ya kutaka Polisi kuzuia mkutano huo kama inavyofanya kwa vyama vingine vya siasa, ilitolewa juzi mjini Moshi na Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Julius Mwita.

Msimamo huo wa Chadema ambao uliungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Salum Mwalim unafuatia Polisi kuzuia mahafali ya wahitimu wa vyuo vikuu ambao ni wanachama wao.

Akizungumza na wanahabari, Mwita alikwenda mbali na kudai kuwa, Chadema watalifungulia Jeshi la Polisi kesi ya madai ya fidia kwa kuvuruga mahafali ya Chaso mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita.

“Ukisoma barua yao wamesema wamezuia mikutano ya hadhara sasa kama wanakuja hadi kwenye vikao vya ndani, hatuwezi kuendelea kukubali jambo hili.Tumetumia busara sana,” alisema Mwita na kuongeza: 

“Msipouzuia Mkutano Mkuu wa CCM Dodoma Julai 23 tunakuja kuuzuia sisi... yaani muwe tayari kusafiri kwenda Dodoma tukauzuie ule mkutano la sivyo, wauzuie kama walivyouzuia mikutano yetu.” 

Mwita alimgeukia Mwalimu na kumweleza kuwa hiyo ni lugha ya ujana na inatekelezeka, akawahoji vijana wa Chaso waliokuwapo: “Wangapi mko tayari kuja Dodoma?” Wote wakaafiki.

“Intelijensia ya polisi ni ya kiumbea, inayoweza kujua tu Chadema wanakwenda kwenye mkutano, haiwezi kujua watu wamejificha wana bunduki na risasi 300 kwenye mawe kule Mwanza,” alidai.

Mwalimu alisema utaratibu wa Polisi na Serikali lazima ukome na kwamba wao ni viongozi.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger