Tuesday, 25 February 2014

ASKOFU BILIONEA BONGO ATIKISA

...

ASKOFU BILIONEA BONGO ATIKISA

Stori: Jelard Lucas
ASKOFU na Nabii George David ‘Geordavie’ wa Kanisa la Geordavie Ministry ‘Ngurumo ya Upako’ lililoko jijini Arusha na Kawe, Dar hivi karibuni alifanya mkutano mkubwa na kutikisa nchi  kwa kuwa na magari ya kifahari na ndege aina ya helikopta ‘chopa’ iliyokuwa ikirandaranda juu ya anga kulinda usalama wake, Uwazi lina ushuhuda wa kutosha.
Katika mkutano huo uliofanyika Karatu mkoani Manyara, mwandishi wetu alishuhudia msafara wa Geordavie ambaye hutoa huduma ya uponyaji kwa njia za miujiza, ukiwavutia watu wengi kwa kuwa ulikuwa na ulinzi mkali ambao haujawahi kutokea.
Mbali ya kuwa na chopa iliyokuwa ikiimarisha ulinzi ambayo ameinunua hivi karibuni, askofu huyo alikuwa na msururu wa magari yenye thamani kubwa yanayomfanya kutajwa kuwa tajiri kuliko maaskofu wengine wanatoa huduma katika makanisa ya kiroho Tanzania.
Akiwa Karatu, mbali na ulinzi binafsi, Geordavie alikuwa akilindwa na askari wa jeshi la polisi, askari kanzu, Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na wale wa usalama barabarani.
Mbali na askari hao wa serikali ambao wamekuwa wakimlinda kila anapofanya mikutano yake, pia Geordavie analindwa na askari wake binafsi hali iliyowafanya baadhi ya watu kuamini kuwa ulinzi wake ni kama ule wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ‘JK’.
“Sijawahi kumuona JK akilindwa na chopa lakini mtumishi wa Mungu Geordavie analindwa na ndege katika msafara wake! Hii ni mara yangu ya kwanza kuona,” alisema muumini mmoja ambaye hakupenda kutajwa gazetini.
Hata hivyo, baadhi ya watu walikuwa wakihoji utajiri wa askofu huyo kutokana na fedha nyingi anazozitumia anapofanya mikutano katika sehemu mbalimbali jijini Arusha.
“Tunajua kuwa ni tajiri, lakini anapata wapi fedha za kutumia hivi?” alihoji muumini aliyejitambulisha kwa jina moja la Julius ambaye naye alihudhuria mkutano wa askofu huyo anayetumia kaulimbiu ya Ngurumo ya Upako katika kutoa huduma yake.
Pia, waumini wengine walilalamikia ugumu wanaoupata wanapotaka  kumuona mtumishi huyo wa Mungu kutokana na ulinzi mkali anaopewa.
“Kila mtu alitamani kumuona mtumishi wa Mungu lakini haikuwezekana kutokana na ulinzi wake kuwa mkali, utajiri wake hakuna mfano, hata kule nyumbani kwake Arusha, anaishi kama Mfalme Daud,” alisema Fred Mushi.
Gazeti hili lilimsaka Askofu na Nabii Geordavie kwa lengo la kutaka kujua sababu ya kuwa na ulinzi mkali na kutumia magari ya kifahari ikiwemo chopa katika mikutano anayoifanya lakini simu yake iliita bila kupokelewa.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger