Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu) Prof. Joyce Ndalichako(kulia) akizungumza na mwekezaji wa kiwanda cha vinywaji cha U-fresh Food Limited (Wapili kushoto) wakati wa ziara yake ya kutembelea maeneo ya kazi katika Mkoa wa Pwani akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sara Msafiri, Viongozi wa Taasisi zilizochini ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na watendaji wengine wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na mwakilishi wa uongozi wa kiwanda cha Kutengeneza bidhaa mbalimbali za usafi cha Keds Tanzania Ltd (wakwanza kulia) pamoja na wafanyakazi wa kiwanda hicho (hawapo pichani) katika ziara yake iliyolenga kufuatilia mrejesho wa utekelezaji wa sheria mbalimbali za kazi Mkoani Pwani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako (aliyesimama) akizungumza na viongozi wa kiwanda cha kuchakata nyama cha Tan Choice Ltd wakati wa kikao cha kutoa tathmini baada ya viongozi wa taasisi zilizochini ya Waziri Mkuu alioambatana nao kukamilisha ukaguzi katika kiwanda hicho.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda (mwenye miwani) akitoa mrejesho wa ukaguzi ulifanywa na wakaguzi wa OSHA katika kiwanda cha vinywaji cha U-fresh Food Limited mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, wawekezaji wa kiwanda hicho pamoja na wafanyakazi wengine kiwandani hapo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako (mbele), Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sara Msafiri (wapili kushoto) Viongozi mbalimbali wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na watendaji wengine wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wakielekea katika maeneo ya kiwanda cha Tan choice yanayofanya uzalishaji wakiongozwa na mwakilishi wa uongozi wa kiwanda hicho kwa lengo la kukagua mifumo ya usalama na afya katika kiwanda hicho.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, akifanya ukaguzi wa shughuli za uzalishaji katika kiwanda cha kuzalisha bidhaa za usafi cha Keds Tanzania Ltd.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha vinywaji cha U-fresh Food Limited wakati wa ziara yake iliyolenga kufuatilia mrejesho wa utekelezaji wa Sheria mbalimbali za kazi ikiwemo Sheria Na 5. Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.
************************
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, amewapongeza wamiliki wa viwanda wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam kwa kutoa ajira kwa maelfu ya Watanzania kupitia uzalishaji wa bidhaa zinazouzwa ndani na nje ya nchi.
Ametoa pongezi hizo alipokuwa akihitimisha ziara yake ya siku mbili (2) katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ambapo ametembelea viwanda na maeneo ya kazi sita (6) yanayozalisha bidhaa mbali mbali vikiwemo vifungashio, vyombo vya majumbani, mabomba, vinywaji, taulo za kike na nyama.
Maeneo yaliyotembelewa na Waziri Ndalichako ni pamoja na Lake Oil Group, Tanzania Ruidar Co. Ltd vya Kigamboni pamoja na Tanchoice Limited, U-fresh Food Limited, Keds Tanzania Ltd na Global Packaging Limited.
Katika ziara hiyo, Waziri Ndalichako ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sarah Msafiri, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Nyangasa, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya (OSHA), Khadija Mwenda, Kamishna wa Kazi, Suzan Mkangwa, watendaji wengine wa Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na Wilaya za Kigamboni na Kibaha.
“Nimehitimisha ziara yangu ya siku mbili katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Lengo la ziara hii ilikuwa ni kupata mrejesho wa utekelezaji wa Sheria za Kazi ikiwemo kuangalia ajira zinazozalishwa na wawekezaji wetu. Jambo la kufurahisha ni kwamba katika maeneo yote sita niliyotembelea nimeona zaidi ya ajira 3,000 zimezalishwa,” amesema Prof. Ndalichako.
Aidha, amesema wengi wao kati ya idadi hiyo yote ni vijana jambo ambalo linadhihirisha kwamba serikali ya awamu tano inatekeleza ipasavyo wajibu wake wa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hapa nchini.
Hata hivyo, pamoja na pongezi hizo kwa wawekezaji, Prof. Ndalichako amebainisha kwamba kumekuwa na dosari ndogo ndogo katika maeneo ya kazi aliyoyatembelea ikiwemo baadhi ya waajiri kutotoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi, kutowasilisha michango katika mifuko ya hifadhi kwa jamii pamoja na baadhi ya maeneo kutokuwa na mifumo madhubuti ya usalama na afya mahali pa kazi.
Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sarah Msafiri, amemshukuru Waziri Ndalichako kwa kufanya ziara katika Wilaya ya Kibaha na kuwakumbusha waajiri kuzingatia Sheria za Kazi ambapo ameahidi kushirikiana na wawekezaji katika kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amewataka wawekezaji kushirikiana kwa karibu na Ofisi yake katika kuboresha mazingira ya kazi.
“Wakati wote sisi tupo tayari kushirikiana nanyi kutengeneza mifumo ya usalama na afya kwenye maeneo yenu ya kazi ili ajira hizi mnazozizalisha kwa wingi ziwe endelevu na zilete tija kwenu, kwa wafanyakazi wenyewe na Taifa kwa ujumla,” amesema Mkaguzi Mkuu wa maeneo ya kazi nchini.
0 comments:
Post a Comment