NA HALIMA KHOYA,SHINYANGA
Mtoto mwenye umri wa miaka 3 (jina limehifadhiwa) mkazi wa mtaa wa dome Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, amedaiwa kubakwa mtu ambaye hakufahamika mara moja katika maeneo ya uchochoroni jirani na nyumbani kwao.
Tukio hilo limetokea jana Oktoba 28, 2022 majira ya saa 4 asubuhi katika mtaa huo wa dome.
Akieleza tukio hilo kwa njia ya simu Mwenyekiti Mtaa wa dome Solomoni Najulwa, amesema taarifa a kubakwa kwa mtoto huyo alipigwa simu na mama yake mzazi, lakini kutokana na yeye kuwa safarini ikabidi atume wajumbe wa mtaa ili wafike eneo la tukio kwa ajili ya kutoa msaada.
Amesema baada ya wajumbe kufika eneo la tukio hawakumkuta mtoto huyo ambapo mama yake mzazi alikuwa tayari ameshampeleka hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu, kutokana na kuumizwa vibaya sehemu zake za siri pamoja na kutoa taarifa Polisi.
Aidha, Najulwa amelaani tukio hilo na kubainisha kuwa katika mtaa wake kumekuwepo na wimbi la vijana wengi wakizurura mtaani na hawana kazi, na ndiyo wamekuwa wakifanya matukio hayo ya ubakaji pamoja na uhalifu, na kuahidi atakomesha vitendo hivyo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
“Majira ya saa 6 mchana nilipigiwa simu na mmoja wa wakazi katika mtaa wangu ambapo aliniambia mtoto wake amebakwa na mtu asiyefahamika, ndipo nilipowatuma wajumbe wafike eneo hilo haraka, ili kutoa msaada kwa mhanga ikiwamo kumpeleka hospitali, lakini walikuta mama yake ameshampeleka,”amesema Najulwa.
“Mimi kama kiongozi wa ulinzi na usalama mtaa wa dome naahidi kushirikiana na wananchi wote kumsakana kwa hali na mali aliyehusika na kitendo cha kikatili kama hiki na tutahakikisha atakayekamatwa anajibu tuhuma zote zilizowahi kutokea kipindi cha nyuma ili kukomesha tabia hii isijitokeze tena”ameongeza.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa Shinyanga ACP Janeth Magomi, amesema bado hajapata taarifa ya tukio hilo na kubainisha kuwa analifuatilia.
0 comments:
Post a Comment