Mkaguzi ( TBS), Anderson Msumanje akitoa elimu ya viwango kwa wadau mbalimbali waliohudhuria maonesho ya SIDO kanda ya kaskazini, Mkoani Arusha. Msumanje alitoa rai kwa wajasiriamali kuanza mchakato wa kuthibitisha ubora wa bidhaa zao kwani Serikali hutenga fedha kwa ajili ya kuwahudumia hivyo huduma hiyo hutolewa bure.Meneja wa Masoko na Uhusiano (TBS) Gladness Kaseka akitoa maelezo kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara - Uwekezaji, Bw Ally Gugu alipotembelea banda la TBS wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 17 ya SIDO kanda ya kaskazini, mkoani Arusha. Gugu amewaasa TBS kuangalia upya vigezo vyao katika kuwahudumia wajasiriamali wadogo kuendana na mazingira yao.
*********************
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetoa rai kwa wajasiriamali kutumia maonesho yaliyoandaliwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido)Kanda ya Kaskazini ili waweze kupata urahisi wa kuthibitisha bidhaa zao na kupata leseni ya kutumia alama yao ya ubora.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika maonesho ya wajasiriamali yaliyoandaliwa na Sido,Mkaguzi wa TBS Kanda ya Kaskazini, Anderson Msumanje alisema maonesho hayo ni fursa kwa wajasiriamali kupata leseni ya kutumi alama ya ubora katika bidhaa wanazozalisha ili iwe rahisi kuuza ndani na nje ya nchi.
Alisema TBS wamewatembelea wajasiriamali zaidi ya 50 na kujua changamoto zao katika kupata alama ya ubora ikiwemo upataji wa jengo la kuzalisha bidhaa zao lakini wanaweza kutumia jengo hilo hilo kwakupanga mtitiriko wa uzalishaji bidhaa vizuri.
Alitoa rai kwa wajasiriamali kote nchini kutuma maombi TBS kwaajili ya kuthibitisha ubora na usalama wa bidhaa na kupata leseni ya kutumia alama ya ubora katika bidhaa zao kwani serikali inatenga fedha kwaajili ya kuthibitisha bidhaa zao hivyo wakipitia Sido watapata fursa mbalimbali za kupata leseni hiyo bila gharama yoyote na TBS itakuwa imewafikia walipo.
"Wafanyabiashara tumieni Sido ili iwaunganishe na TBS lengo ni kufungua milango ya biashara baada ya kuthibitisha ubora na kufungua masoko ndani na nje ya nchi"
Naye mmoja kati ya wafanyabishara aliyepata leseni ya kutumia alama ya ubora ya TBS, Christina Macha alitoa rai kwa wajasiriamali kutokuikimbia TBS bali wawe karibu na shirika hilo ili kupata maelekezo ya kupata alama za ubora kwani mimi nilifuata vigezo na TBS walinikagua na sasa baadhi ya bidhaa zangu zimepata alama ya ubora
"Msiogope TBS wala kuikimbia itumieni ili biashara zenu zifike mbali zaidi, sasa hivi bidhaa zangu nafungasha vizuri na ninaweza kuziuza hata nje ya nchi"
Huku Meneja Masoko wa kampuni ya Sessan Skin Care,Christen Mushi alisema wanatumia maonesho hayo kwaajili ya kuuza bidhaa zao ikiwemo asali na aliishukuru TBS kwajitihada wanazofanya kwaajili ya kuwafikia wajasiriamali wadogo na wakubwa katika kuhakikisha bidhaa wanazozalisha zinakuwa na ubora.
Maonesho hayo yalianza Oktoba 19-10-2022 na yameshirikisha wajasiriamali kutoka mikoa ya kanda ya kaskazini.
0 comments:
Post a Comment