Na Mwandishi wetu,KIGOMA..
SERIKALI kupitia mkopo wa Benki ya Dunia imetenga kiasi cha dola za Marekani milioni 45.5 kwa ajili ya ujenzi wa kampasi ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) ambapo kati ya fedha hizo, kiasi cha dola za Marekani milioni 15 zitatumika kwenye ujenzi wa miundombinu katika kampasi ya Kigoma.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo 17 Octoba 2022 Wilayani Kasulu wakati wa ziara ya kikazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Mkoani Kigoma na kueleza kuwa Kampasi hiyo itajengwa katika Halmashauri ya Ujiji mkoani Kigoma.
Amefafanua kuwa "Kampasi hiyo itajengwa katika eneo la ekari 47.3 ambalo linapakana na eneo litalojengwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Magharibi,Kampasi hii inatarajiwa kuwa na miundombinu itakayotoa mazingira bora ya ufundishaji na kujifunzia, utafiti pamoja na utoaji wa huduma kwa jamii,"amesema
Waziri huyo pia amemshukuru Rais Samia kwa kuzindua majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Kabanga ambayo ni moja kati ya Miradi iliyotekelezwa na Wizara ikiwa ni Mkakati wa Serikali wa kuboresha Mazingira ya utoaji wa Elimu ya Ualimu nchini.
Prof. Mkenda amesema kuwa Ujenzi huo umefadhiliwa na Serikali ya Canada kupitia Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu nchini (Teachers Education Supports Project – TESP).
Mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga ulianza tarehe 26/03/2019 na ulikamilika tarehe 22/04/2022.
Ujenzi umetekelezwa na Mkandarasi SUMA JKT Kanda ya Magharibi chini ya Usimamizi wa Mshauri Elekezi Bureau for Industrial Cooperation (BICO) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Aidha, kazi ya utengenezaji na uwekaji wa Samani katika majengo haya inaendelea.
0 comments:
Post a Comment