Tuesday, 12 July 2022

WAZIRI WA NISHATI AANZA UHAMASISHAJI WA MATUMIZI SAFI YA NISHATI NCHINI

...

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba (wa Tatu kutoka kulia) akizungumza na Mwakilishi wa Kikundi cha Kusama, Bi.Beatrice Mbaga kuhusu athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya mkaa na kuni wakati akiwa wilayani Musoma, mkoani Mara ambapo alikabidhi mitungi Sita ya Gesi na kuahidi kufunga mfumo wa gesi kwa kikundi hicho ambacho kinatumia kuni na mkaa kukaanga dagaa.

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba (kushoto) akizungumza na Bi.Tereza Stephano wa Kijiji cha Kisamwene wilayani Butiama kuhusu athari za matumizi ya kuni na mkaa katika mfumo wa upumuaji pamoja na faida za kutumia nishati safi ya kupikia. Waziri wa Nishati aligawa mtungi wa Gesi kwa kaya ya Bi. Tereza Stephano ili iweze kutumia kwa matumizi ya kupikia.

Waziri wa Nishati, January Makamba akizindua mradi wa umeme wa BUTUGURI wilayani Butiama mkoani Mara ambao utasambaza umeme katika Nyumba 287 na utagharimu Shilingi milioni 385. Mradi huu utawasaidia wananchi kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kufunga mashine za kusaga na kukoboa nafaka, uchomeleaji na upatikanaji wa huduma bora za kijamii ikiwemo maji baada ya umeme kufika katika miradi ya maji.

Bi.Tereza Stephano kutoka Kijiji cha Kisamwene wilayani Butiama mkoani Mara akimshukuru Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba baada ya kumkabidhi mtungi wa gesi utakaomwezesha kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo yanaleta athari katika mfumo wa upumuaji. Kulia kwa Waziri wa Nishati ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini ambaye pia ni Mbunge wa Butiama.

Dkt. Mary Mahenge kutoka Hospitali ya Mkoa wa Mara iliyopo wilayani Musoma akimweleza Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba ( wa Pili kutoka kushoto) kuhusu magonjwa ya mfumo wa hewa ni yanayotokana na kuchomwa kwa kuni na mkaa wakati Waziri wa Nishati alipofanya ziara mkoani Mara kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

………………………..

Ikiwa ni utekelezaji wa moja ya vipaumbele vya Wizara ya Nishati katika Bajeti ya mwaka 2022/2023, Waziri wa Nishati, January Makamba ameanza kazi ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika mikoa mbalimbali nchini ambapo Awamu ya kwanza ya uhamasishaji inayojumuisha mikoa 14 na Wilaya 38 imeanzia mkoani Mara.

Katika siku ya kwanza ya kazi, Waziri wa Nishati, alizungumza na makundi mbalimbali ya wananchi katika Wilaya za Musoma, Butiama na Bunda na kugawa mitungi ya Gesi kwa vikundi mbalimbali pamoja na kaya maskini.

“Sisi kama Wizara ya Nishati moja ya mambo tunayosimamia ni nishati ya umeme, nishati ya kupikia na ya kwenye magari ila nishati ya kupikia tumekuwa hatuigusi, lakini hii ni nishati ambayo kila mtanzania lazima atumie, hivyo kuanzia mwaka huu, tumeamua kutoa kipaumbele kikubwa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.” Alisema Makamba

Alieleza kuwa, kwa hapa Tanzania wananchi takriban Elfu 22 wanakufa kwa mwaka kutokana na magonjwa ya njia ya kupumua yanayosababishwa na kutumia mkaa na kuni ambapo kwa Mkoa wa Mara takriban wananchi 400 hadi 600 huugua kwa mwaka kutokana na matumizi hayo hivyo athari hizo pia zinaipa msukumo Serikali katika kuwahamasisha wananchi kutumia nishati safi.

Kuhusu changamoto za bei ya gesi ya mitungi ambayo inafanya wananchi wengi kuendelea kutumia kuni na mkaa, alieleza kuwa Serikali inachukua hatua mbalimbali ikiwemo kupunguza kodi ili familia mbalimbali ziweze kumudu bei ya mitungi ya gesi.

Suala la athari za matumizi ya kuni na mkaa, lilitiliwa mkazo na Dkt. Mary Mahenge kutoka Hospitali ya Mkoa wa Mara iliyopo wilayani Musoma ambaye alieleza kuwa, kwenye nchi zinazoendelea, sababu kubwa ya magonjwa ya mfumo wa hewa ni kuchomwa kwa kuni na mkaa na kwamba kinacholeta madhara kwenye matumizi hayo ni moshi ambao una hewa ya carbonmonoxide ambayo ikiwa nyingi inaweza kusababisha pia vifo vya ghafla.

Akiwa wilayani Musoma alikabidhi mitungi Sita ya Gesi kwa Kikundi cha Kusama ambacho kinakaanga dagaa kwa kutumia kuni na mkaa pamoja kuahidi kufunga mfumo wa gesi ambao utasaidia kikundi hicho kufanya kazi kwa ufanisi.

Mwakilishi wa Kikundi cha Kusama, Bi.Beatrice Mbaga ambaye alisema macho yake yameathirika kutokana na kupikia kuni kwenye biashara hiyo kwa miaka 17, alimshukuru Waziri wa Nishati, January Makamba kwa ahadi aliyoitoa ya kufungiwa mfumo wa gesi ambao utahamasisha pia vikundi vingine vya wajasiriamali kutumia nishati safi kwenye kazi zao.

Aidha, akiwa wilayani Butiama katika Kijiji cha Kisamwene, aligawa mtungi wa Gesi kwa kaya maskini ya Bi. Tereza Stephano ambaye alimshukuru Waziri wa Nishati kwa kupata nishati hiyo safi ya kupikia ambayo itamrahisishia shughuli za upishi huku akiwa na uhakika wa usalama wa afya ya familia yake.

Pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi mkoani Mara, akiwa wilayani Butiama, Waziri wa Nishati alizindua mradi wa umeme wa Butuguri ambao utasambaza umeme katika kaya 287 na utagharimu shilingi milioni 385 ambapo mradi huo utawawezesha wananchi wa eneo hilo kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi ikiwemo kujiajiri.

Pia, Waziri wa Nishati alizindua huduma ya Ni-Konekt kwa Mkoa wa Mara ambapo huduma hiyo inawawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na TANESCO kwa njia ya mtandao ikiwemo maombi ya kuunganishiwa umeme.

Ziara ya Waziri wa Nishati iliyoanza tarehe 11 Julai 2022, itakuwa ni ya siku 21 ambapo atahamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na kukagua miradi mbalimbali ya nishati katika Mikoa 14, Wilaya 38 na Majimbo 41.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger