Mwanaume mwenye umri wa miaka 30, amezikwa akiwa hai Jumatatu, Julai 25, akichimba choo katika Shule ya Sekondari ya Jean Marie, Kaunti ya Nandi nchini Kenya.
Josphat, ambaye alikuwa miongoni mwa wanaume watatu waliopewa kandarasi ya kuchimba choo katika shule hiyo, alikwama baada ya kuta za choo hicho kuporomoka akiwa ndani mwendo wa saa nane kamili mchana.
Nicholas Odungo, ambaye alikuwa sehemu ya kikosi hicho cha uchimbaji alisema kisa hicho kilitokea wakati watatu hao walikuwa wakimalizia kazi yao.
Choo kilikuwa cha futi 30. Odungo na wenzake walikuwa wamekwenda kupata chamchana wakati tukio hilo lilitokea.
"Tulikuwa tumeenda kula chakula cha mchana na tukamwambia aendelee kuchimba. Tulirudi muda mfupi baadaye ili kumsaidia kuondoa udongo na tukiwa katika harakati za kufunga kamba kuta zikazama," Odungo alisema kama alivyonukuliwa na K24.
Josephat, baba wa watoto watatu bado amekwama kwenye vifusi huku juhudi za uokoaji zikiendelea. Wakaazi wenye mfadhaiko sasa wanatoa wito kwa serikali ya kaunti na ya kitaifa kusaidia katika juhudi za uokoaji.
“Inasikitisha sana kwamba tulikuwa tunamalizia kazi yetu kabla hatujalipwa lakini kilichotokea kimetuathiri sana, tunaomba kikosi cha uokoaji na wasimamizi wa maafa waje kumuokoa Josphat ambaye amenaswa tangu saa 2:00 usiku," mkazi mmoja alisema.
Chanzo - Tuko news
0 comments:
Post a Comment