Monday, 18 July 2022

IJA YAENDESHA MAFUNZO ELEKEZI KWA WATUMISHI WA MAHAKAMA

...

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbard Chuma akifungua mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wa Mahakama ya Tanzania yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Picha mbalimbali za watumishi wapya wa Mahakama ya Tanzania wakifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka wa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbard Chuma.

………………………………………………

Mhe. Wilbard Chuma Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania leo tarehe 18/07/202 amefungua rasmi mafunzo elekezi kwa watumishi wapya 58 wa Mahakama Tanzania. Mafunzo hayo yanaendeshwa na kufanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA). Hili ni kundi la kwanza kati ya waajiriwa 227 waliofanyiwa usaili na kuajiriwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama hivi karibuni ambapo kuna kada mbalimbali kama Mahakimu, Maafisa Utumishi, Maafisa TEHAMA, Makatibu Mahususi, Watunza Kumbukumbu Wasaidizi na Madereva.

Akitoa hotuba ya ufunguzi, Mhe. Chuma alianza kwa kuwapongeza waajiriwa hao wapya kwa kuwaeleza kuwa ajira waliyopata hawakupata kama hisani ila imepatikana kutokana na ubora waliouonesha wakati wa usaili hivyo wanapaswa kuwa waaminifu, waadilifu na wachapakazi kwa kuzingatia mikataba ya ajira, viapo na sheria za nchi katika utumishi wao.

Mhe. Chuma aliendelea kwa kuwasisitiza Watumishi hao wapya wa Mahakama kwa kumnukuu Jaji Mkuu wa Mahakama wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe Mei 31, 2021 katika hotuba yake aliyoitoa wakati akifungua rasmi Mafunzo elekezi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na Mahakama Kuu Zanzibar hapa Chuoni kwa kusema watumishi wa Mahakama wanatakiwa kuwa na uadilifu na maadili ili wafanye kazi kwa kuzingaia Katiba na masharti ya viapo.

“Watu husahau kuwa mara nyingi sheria sio mbaya bali ni nafsi, maadili na tabia za wanaotekeleza sheria hizo. Hivyo nawakumbusha kila jalada utakalokuwa ukilitolea uamuzi ukumbuke kuwa linagusa watu halisi, linagusa uhuru wao, biashara zao, mali zao na familia zao. Kumbukeni kuwa wananchi kupitia katiba wametupa sisi Majaji mamlaka ya utoaji haki lakini wananchi wamebaki na haki zao zote za msingi” alinukuu.

Mhe. Chuma aliendelea kwa kuwakumbusha watumishi hao kuwa maadili ni kiini cha haki, na hivyo wakati wa kutekeleza jukumu la utoaji haki na wanatakiwa kuzingatia maadili ya kazi na kutoa maamuzi kwa kuzingatia misingi ya haki, sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.

Mhe. Chuma aliwaeleza watumishi hao wapya kuwa malengo ya mhimili wa Mahakama yatafikiwa iwapo watakuwa na nia moja na ushirikiano baina yao na watumishi wengine watakaowakuta kwenye vituo vya kazi watakavyopangiwa. Alieleza kwamba ushirikiano huo utasaidia kufanikisha jitihada zinazoendelea za maboresho ya Mahakama ya Tanzania. Mhe. Chuma aliwasisitiza watumishi hao kuwa na ushirikiano na wadau wengine kwa kuchukua mawazo mazuri na bora kutoka kwenye taasisi au idara zingine kwa kuyafanyia kazi au kuyafikisha mahali panapostahili ili yalete mabadiliko kwa kuwa kazi ya kulijenga taifa ni wote.

Mhe. Chuma aliendelea kwa kuwasisitiza watumishi hao kuwa dhana ya uhuru wa mahakama haina maana ya kuvunja sheria kwa kuwa kanuni hii ya kikatiba inaenda sanjari na kanuni ile ya Utawala wa Sheria. Hivyo, amewataka Mahakimu kuwa ni wajibu wao kufanya kazi zao chini ya kivuli cha uhuru wa Mahakama, kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria za nchi na sio kwa kuzivunja. Aliendelea kwa kuwaasa watumishi wengine ambao sio mahakimu wakawasaidie maafisa wa Mahakama wa ngazi mbalimbali katika kufikia azma ya kutenda na kutoa haki kwa mujibu wa sheria ili wasiwe chanzo cha malalamiko au kusababisha uvunjifu wa amani kutokana na utendaji kazi ambao unakiuka misingi ya utu na katiba.

Mafunzo haya yanafanyika kwa makundi matatu ambapo kundi la kwanza la Mahakimu Wakazi na Maafisa Kumbukumbu Wasaidizi yamenza leo tarehe 18 Julai ,2022. Makundi mengine ya kada nyingine yatafuata na kutegemea kumalizika 12 Agosti, 2022.

IJA inajukumu la kuwajengea uwezo watumishi wote wa mahakama kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wao pia kwa mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali yanayotoa huduma za utoaji haki nchini. Pamoja na mafunzo hayo Chuo kimebobea katika kutoa mafunzo ya Stashahada na Astashahada ya sheria. Vilevile Chuo kinafanya shughuli za kutoa ushauri wa kitalaamu, machapisho na tafiti mbalimbali.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger