Mwezeshaji wa mafunzo ya usalama na afya kutoka OSHA, Respicious Kundawa , akitoa mafunzo kwa wafanyakazi wa kiwanda cha PNP Industries Limited.
Mwezeshaji wa mafunzo ya usalama na afya kutoka OSHA, Respicious Kundawa , akizungumza na mmoja ya washiriki wa mafunzo wa kiwanda cha PNP Industries Limited. OSHA imetoa mafunzo hayo kuwawezesha wafanyakazi kujilinda dhidi ya vihatarishi wanapokuwa kazini.
Mwezeshaji wa mafunzo ya usalama na afya kutoka OSHA, Respicious Kundawa , akitoa maelekezo kuhusu kuboresha mazingira ya kazi kwa wasimamizi wa wafanyakazi wa kiwanda cha PNP Industries Limited mara baada ya kutoa mafunzo ya usalama na afya kiwandani hapo.
Wafanyakazi wa kiwanda cha PNP Industries Limited wakifuatilia mafunzo ya usalama na afya yaliyotolewa na OSHA kiwandani hapo. Mafunzo hayo yalilenga kuwawezesha wafanyakazi kujilinda dhidi ya vihatarishi wanapokuwa kazini.
******************************
Na Mwandishi Wetu
Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umetoa mafunzo maalum ya usalama na afya kwa wafanyakazi wa kiwanda cha kuzalisha nondo cha PNP Industries Limited yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kujilinda dhidi ya ajali na magojwa yanayotokana na mazingira yao ya kazi.
Mwezeshaji wa Mafunzo hayo kutoka OSHA, Respicious Kundawa, amesema mafunzo hayo ni muhimu hususan kwa wafanyakazi wanaohusika moja kwa moja katika mchakato mzima wa uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu.
“Katika mafunzo ya leo tumewalenga wafanyakazi katika viwanda vya kuzalisha nondo ambao tunafahamu wanakabiliwa na vihatarishi mbali mbali katika mlolongo mzima wa uzalishaji wa bidhaa husika kuanzia wanapopokea vyuma chakavu, kuvichambua, kuviyeyusha, kutengeneza nondo zenyewe na hata kuzipakia katika magari tayari kwa kuzisafirisha kwenda kutumika,” alieleza Kundawa.
Aliongeza: “Katika hatua zote hizo mfanyakazi anaweza kuumia hivyo ni muhimu kuwapa wafanyakazi nyenzo za kujilinda.”
Kwa upande wa uongozi wa kiwanda hicho umeeleza kuridhishwa na mafunzo yaliyotolewa na OSHA na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa kupitia mafunzo hayo.
“Tunashukuru OSHA kwa mafunzo waliyotupatia kwa siku ya leo ambayo yatatusaidia sana katika kuboresha mazingira yetu ya kazi pamoja na namna ambavyo tunafanya kazi,” alisema Iddy Hamis, Afisa Rasilimali Watu wa Kiwanda cha PNP Industries Limited.
Aidha, wafanyakazi walioshiriki katika mafunzo hayo wamesema akiwemo Juma Kajembe na Solomon Lukas wamesema mafunzo waliyoyapata yatasaidia katika kuboresha namna ambavyo wamekuwa wakitekeleza majukumu yao na hivyo kujiepusha na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.
“Tunashukuru kwa mafunzo tuliyoyapata kwa siku ya leo, tunaimani yatatutoa kutoka hatua moja kwenda nyingine kahusiana na usalama wetu tuwapo kazini. Kwasasa tunaweza kutambua vitu gana ni hatarishi katika maeneo yetu kazini pamoja na matumizi sahihi ya vitendea kazi na vifaa kinga,” alisema Juma Kajembe ambaye ni mfanyakazi wa kiwanda cha PNP.
Mafunzo hayo ambayo yamefanyika katika eneo la kiwanda, Mikocheni jijini Dar es Salaam, yamejumuisha wafanyakazi zaidi ya 90 ambao wanahusika na shughuli mbali mbali katika mlolongo mzima wa uzalishaji nondo pamoja na wasimamizi wao.
Wakati huo huo, OSHA imehitimisha darasa la mafunzo ya usalama na afya katika sekta ya mafuta na gesi yaliyofanyika katika ofisi za OSHA ambayo yalijikita katika kuwaandaa wataalam ambao watatumika kusimamia usalama wa wafanyakazi katika miradi ya mafuta na gesi inayotarajiwa kuanza kutekelezwa hapa nchini.
0 comments:
Post a Comment