Thursday, 27 May 2021

POLISI SHINYANGA WAKAMATA MATAPELI WANAOGHUSHI NYARAKA, KUTONGOZA NA KUIBIA WANAWAKE

...

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linawashikilia watuhumiwa watatu  Dismond Zacharia  (33) ambaye ni mwalimu, Feisal Hussein  (27) Mpemba, mtaalamu teknolojia ya mawasiliano, Juma Almas (35) Mfanyabiashara baada ya kuwakamata wakiwa na nyaraka mbalimbali za kughushi kwa lengo la kutapeli Wananchi. 

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Mjini Kahama, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema  watuhumiwa hao walikamatwa Mei 26, 2021 majira ya saa 07:00 asubuhi huko maeneo ya Namanga Manispaa ya Kahama.

Amesema watuhumiwa hao wamekamatwa kufuatia msako mkali unaoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga wa kupambana na uhalifu na wahalifu.

"Baada ya watu hao kukamatwa na kufanyiwa upekuzi walikutwa na vitambulisho viwili vya Jeshi la wananchi (JWTZ), kitambulisho cha Idara ya Usalama wa Taifa (TISS),  Mhuri mmoja wa Jeshi la Wananchi Tanzania pamoja na nyaraka mbalimbali za Jeshi hilo. Orodha ya nyaraka hizo ni barua za utambulisho kwenye mabenki, ripoti za Jeshi la Wananchi, fomu za kusafirishia mizigo ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ)",amesema Kamanda Magiligimba. 

Kamanda Magiligimba amesema watuhumiwa hao wanatumia mbinu mbalimbali kufanya utapeli huo kama vile kufika kwa watoa  huduma za kifedha mikoa mbalimbali kwa kutumia magari (T.677 BMA Toyota  Carina namba  T.110 DSX Toyota RUMION) na kuulizia ofisi za viongozi wa Serikali na pindi wanapoonyeshwa hushusha begi linalosadikiwa kuwa na fedha na kuliacha kwa wakala aliyewekeza ili hali begi hilo likiwa na makaratasi yaliyokatwa mithili ya fedha na kuweka fedha juu na chini ya vibunda vya makaratasi hayo.

 "Na baada ya muda hurudi na kufungua begi na kutoa shukrani kuwa fedha wamezikuta salama na baada ya hapo huja tena baada siku moja na kuacha tena begi na kuelekea kwenye hizo ofisi tena na huomba kurushiwa fedha kuanzia Tshs.500,000/= na kwamba watazirudisha watakapokuja kuchukua begi na huzirejesha na kuchukua begi,  baada ya hapo huja tena na kuacha begi na kuomba kutumiwa fedha  kuanzia milioni moja 1,000,000/= na kuendelea na kuahidi kuzirejesha watakapoijia begi pindi wakirushiwa pesa hizo hutokomea na mtoa huduma anapofungua begi hukuta ni makaratasi na simu zao zinakuwa zimezimwa",ameeleza.

"Mbinu nyingine wanayotumia ni kutongoza wanawake na kuwanywesha Pombe kisha kuwaibia fedha na simu zao pamoja na vitu vya thamani",ameongeza.

Amesema watuhumiwa hao pia hujitambulisha kuwa wao ni maofisa wa Serikali kutoka Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na kuwaahidi kuwapatia ajira.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga anatoa wito kwa Wananchi kuwa makini na mtandao huo wa matapeli na yeyote mwenye taarifa za matapeli wa aina hiyo au aina yeyote ile anaombwa kuzifikisha haraka katika kituo cha Polisi kilicho karibu ili waweze kushughulikiwa haraka kabla hawajaleta madhara kwa jamii.

Pia anasisitiza Wananchi wachache wenye tabia kama hizo za utapeli kuacha mara moja na wafanye kazi halali ili wajipatie kipato halali kwa ustawi wa Mkoa wetu na Taifa kwa ujumla.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger