Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameliagiza Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) liimarishe usimamizi na kuvisaidia vyuo kutoa elimu inayozingatia viwango vya ubora na vyenye kukidhi mahitaji ya soko ya ajira la sasa na lijalo.
Amesema kuwa ni wajibu wa vyuo hivyo kuhakikisha vinatoa elimu bora ili kuwafanya wahitimu wake wawe mahiri na kukidhi mahitaji ya nchi na pia kuwawezesha kujiajiri wao wenyewe.
Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Mei 28, 2021) wakati akifungua Maonesho ya Pili ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Amesema kuwa vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi vinapaswa kutumia fursa ya maonesho hayo kujitathmini na kujipima ili kuona ni kwa namna gani vinaweza kutoa Elimu na Mafunzo ya Ufundi bora yanayokidhi mahitaji ya sasa ya soko la ajira na kutoa fursa kwa vijana kujiajiri.
“Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 imeweka wazi kuwa elimu ni kipaumbele cha juu kwani ndiyo kitovu cha kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwenye jamii”.
Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa ulimwenguni kote elimu na mafunzo ya ufundi na ufundi stadi hujulikana kwa mchango wake mkubwa katika ukuaji wa maendeleo ya viwanda, uchumi na ustawi wa jamii. “Vyuo na taasisi zinazotoa elimu hii ni lazima vihakikishe vinatoa elimu bora inayokidhi viwango na mahitaji ya soko la sasa la ajira”
Kadhalika, Waziri Mkuu aliongeza kuwa Serikali kwa upande wake itaendelea kuweka sera ambazo zinatoa fursa kwa wadau mbalimbali kuwekeza katika sekta ya elimu na hivyo, kuunga mkono juhudi za kuliletea Taifa maendeleo.
“Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za umma na binafsi ambazo zinatoa Elimu na Mafunzo ya Ufundi hapa nchini. Hivyo, natoa wito kwa wadau wote kuungana na Serikali kuwekeza katika utoaji wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika fani mbalimbali”
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa Wizara itaendelea kuhakikisha inatoa elimu ya mafunzo ya ufundi kwa kuzigatia mahitaji ya soko ya kipindi husika na kuwaandaa vijana kwa siku zijazo.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uongozi NACTE Prof. John Kondoro amesema kuwa watashirikiana na vyuo, taasisi za elimu ya mafunzo ya ufundi na wadau wengine kusimamia utoaji wa mafunzo na kuhakikisha elimu ya ufundi na mafunzo inatolewa kwa ubora ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira la ndani na nje.
(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
0 comments:
Post a Comment