Watu watano wakazi wa Mkoa wa Katavi na Rukwa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kukutwa na vipande vinne vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh34.6 milioni.
Washtakiwa hao waliosomewa mashtaka yao na wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Saimon mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi, Kassian Matembele ni Craft Kileo, Godfrey Kashuli, Richard Kafwa, Moses Zakaria na Benjamin Lushina.
Kabla ya kusomewa mashtaka yao, Matembele aliwaeleza kuwa hawatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.
Akiwasomea mashtaka yao, Simon amedai katika shtaka la kwanza linalomkabili Kileo na Kashuli inadaiwa Mei 5, 2021 wakiwa eneo la Ukonga Wilaya ya Ilala walikutwa na vipande vinne vya meno ya tembo ambavyo ni mali ya Serikali bila kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori.
Katika shtaka la pili linalowakabili washtakiwa wote inadaiwa kati ya Aprili Mosi, 2021 na Mei 5, 2021 wakiwa eneo la Katavi na Dar es Salaam walisafirisha vipande vinne vya meno hayo bila kibali cha mkurugenzi huyo.
Baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili, Matembele aliwaeleza kuwa mahakama hiyo haiwezi kuwapa dhamana kwa sababu sheria inaeleza kuwa thamani ya mali ikizidi Sh10 milioni, dhamana inatolewa na mahakama kuu, kwamba kama wanataka dhamana wakaombe katika mahakama hiyo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 8, 2021 na washtakiwa wamerudishwa rumande.
0 comments:
Post a Comment