Thursday, 27 May 2021

Majaliwa: Tutaendelea Kusimamia Bei Nzuri Ya Mazao

...

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan itaendelea kusimamia bei nzuri ya mazao kwa wakulima nchini.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Mei 27, 2021) wakati akijibu swali la Mbunge wa Kyerwa Innocent Bilakwate katika kipindi cha Maswali ya Papi kwa Papo kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma.

Mbunge huyo alitaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuhakikisha zao la Kahawa linakuwa na soko la uhakika.

"Kahawa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati ambayo yanalimwa na jamii pana hivyo Serikali itaendelea kusimamia ushirika, masoko ili wakulima waweze kulipwa kwa wakati".

Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa pamoja na kutafuta changamoto ya  masoko, pia Serikali imeendelea kutekeleza mkakati wa uanzishwaji wa viwanda ndani ya nchi ili zao la kahawa liweze kuongezewa thamani na kuwa na masoko ya uhakika.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha inawalinda raia na mali zake ili wanaendesha kazi zao kwa amani na utulivu.

"Hata Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kupitia hotuba yake moja ya kitaifa, amewaonya wote wanaofikiria huu ni wakati wa kufanya maovu nchini na amewataka wote wanaofikiria kufanya hivyo waache mara moja, haya pia ni maagizo kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua wote wanaosababisha madhara ya usalama kwa watanzania"

Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa watanzania kushiriki katika suala la ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa kila wanapoona kuna dalili za uvunjifu wa amani katika maeneo yao ili majeshi yaweze kufanya kazi iliyokusudiwa.

Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu Swali la Mbunge wa Makete, Festo Sanga aliyetaka kujua  kuhusu mkakati wa Serikali katika kuthibiti vitendo vya uhalifu nchini ikiwemo ujambazi.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa mkakati wa ujenzi wa viwanda nchini umelenga kuhakikisha nchi inapunguza changamoto ya ajira kwa Watanzania wa ngazi zote za elimu kwa sababu kwenye viwanda kuna kazi nyingi kwa watu wa kada zote.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha vyuo vya ufundi stadi ili kuwawezesha Watanzania kupata ujuzi wa kujiajiri.  "Katika miaka mitatu iliyopita tumeweza kukusanya vijana zaidi ya 35,000 tukawapeleka kwenye sekta mbalimbali".

Akijibu swali la Mbunge wa Nkasi, Aida Kenani aliyetaka kufahamu kuhusu  mkakati wa Serikali wa  kutoa huduma za magonjwa ya kisukari kuanzia ngazi ya wilaya hadi kata, Waziri Mkuu amesema kuwa kwa sasa huduma za ugonjwa wa kisukari zinatolewa mpaka ngazi ya zahanati kama sera ya afya inavyoelekeza.

"Halmashauri zote ambazo ndizo zinasimamia Zahanati hakikisheni mnaagiza dawa za kisukari na ziende kwenye zahanati na vituo vya afya ili Watanzania wapate huduma hiyo bila ya usumbufu wa  kusafiri"

 Wakati huohuo Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imejipanga kupambana na majanga mbalimbali ili shughuli za watanzania ziwende kwenda vizuri “tumeendelea kukiimarisha kitengo cha maafa ili kukabiliana na majanga kwa kuweka vifaa, kuwa na wataalamu pamoja kupeleka elimu kwa wananchi kushughulikia majanga pindi tu yanapotokea”

MWISHO.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger