Saturday 15 May 2021

OFISI YA WAZIRI MKUU YASHEREKEA EID NA WANAFUNZI WENYE ULEMAVU

...

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe.Ummy Nderiananga akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Yombo ambacho ni maalum kwa watu wenye ulemavu
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Jamal Katundu akieleza jambo wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Watu wenye Ulemavu Yombo, Jijini Dar es Salaam
Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akitoa mkono wa Idd kwa baadhi ya wanachuo wa Chuo cha Ufundi Stadi Yombo, alipoambataana na viongozi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kwenda kushiriki chakula cha mchana na wanachuo hao katika kusherekea sikukuu ya Eid El Fitr
Wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Yombo ambacho ni maalum kwa watu wenye ulemavu, wakiwasikiliza viongozi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ambao walikwenda chuoni hapo kwa lengo la kula nao chakula cha mchana katika kusherekea sikukuu ya Eid El Fitr.

*******

Na Mwandishi Wetu

Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa chakula cha mchana na kushiriki pamoja na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Yombo ambacho ni maalum kwa watu wenye ulemavu katika kusherekea sikukuu ya Idd El Fitr.

Akimwakilisha Waziri Mkuu katika tukio hilo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga, amesema lengo la kuandaa chakula hicho ni kuendeleza umoja na kutoa faraja kwa kundi hilo la watu wenye ulemavu.

Katika kusherekea sikukuu hii ya Idd El Fitir, Ofisi ya Waziri Mkuu iliona ni muhimu kuandaa chakula cha mchana na kushiriki pamoja na vijana wetu wa chuo hiki cha watu wenye ulemavu hivyo Waziri Mkuu pamoja na Waziri wetu wa Nchi, Mhe. Jenista Mhagama wamenituma niwawakilishe katika tukio hili kwasababu wao wapo katika majukumu mengine ya kitaifa, amesema Ummy Nderiananga.

Naibu Katibu Mkuu katika Wizara hiyo, Prof. Jamal Katundu, ametoa wito kwa taasisi na watu binafsi kujenga utamaduni wa kuyajali na kuyasaidia makundi mbali mbali ya watu wenye mahitaji maalum kikiwemo chuo hicho cha watu wenye ulemavu.

Hili jambo kubwa sana na ndio maana mimi kama Naibu Katibu Mkuu nimepewa jukuma la kuratibu suala hili na kama mlivyoona vijana wetu wamefurahishwa sana na tukio hili hivyo natumie fursa hii kutoa wito kwa watu wenye uwezo na taasisi mbali mbali zenye mafungu ya kusaidia jamii kuona ni kwa jinsi gani wanaweza kuja kuwasaidia vijana wetu, Prof. Jamal Katundu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Mariam Chelangwa, amesema menejimenti pamoja na wanachuo wamelipokea tukio hilo kwa furaha sana ambapo ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuandaa tukio hilo.

Aidha, baadhi ya wanachuo wakiwemo Joseph Baraza na Evodia Mwombeki wameelezwa kufurahishwa na tukio hilo na wameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na viongozi mbali mbali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ambao walijumuika nao katika chakula hicho.

Tumefurahi sana kwa namna moja ama nyingine kwasababu huwa tunajisikia furaha sana kujumuika na watu tofauti tofauti na kujiona kwamba hatujatengwatunawashukuru sana kwa tukio hili la leo na Mungu awabariki sana, amesema Evodia Mwombeki, Mwanafunzi katika fani ya Kilimo na Ufugaji.

Chuo cha Ufundi Stadi Yombo cha watu wenye ulemavu ambacho kipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kilianzishwa mwaka 1973 kwa malengo ya kutoa mafunzo ya ufundi kwa vijana wenye ulemavu nchini. Kwasasa kina jumla ya wanafunzi 76 na kinatoa kozi mbali mbali zikiwemo; Ufundi Umeme, Uwashi, Ushonaji, Uchomeleaji Vyuma pamoja na Kilimo na Ufugaji.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger